Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani taasisi mbalimbali zimetakiwa kuhakikisha wanatoa huduma katika hali ya usawa bila kubagua jinsia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Akiba Commercial Bank (ACB)  Rukia Adam wakati wa kuwashukuru wateja wao waliokuwa nao kwa kipindi kirefu.

Amesema, kauli ya mbiu ya mwaka huu ni “Uwajibikaji wa Uongozi katika kujenga Kizazi cha Usawa wa Jinsia” ina maana kubwa sana na inawakumbusha taasisi zote za kifedha  na nyingine kuhakikisha wanawake wanapatiwa fursa kubwa za ajira.

Rukia amesema, wanatambua mchango wa wanawake katika kujenga jamii bora ndio maana zaidi ya asilimia 50 ya wateja wanaopata huduma kwenye benki yao ni wanawake.

"Asilimia 50 ya wateja wetu ni wanawake ambao wamewezeshwa kwa kupewa huduma mbalimbali ambazo zimewasaidia kubadilisha hali zao za maisha kwa kuwa na maisha bora,"amesema Rukia.

Ameeleza, ACB ni watekelezaji wazuri wa maswala ya usawa wa Kijinsia katika ngazi zote, tunao uwakilishi mzuri wa akina mama kwenye bodi ya wakurugenzi, menejimenti na kiujumla wametoa ajira kwa wanawake aslimia 61 ukilinganisha na wanaume asilimia 39.

Naye, Salma Rashid Ally mteja wa benki hiyo kwa kipindi cha miaka 20, amesema amekuwa mteja wa ACB kwa kipindi kirefu na ameweza kujiendelea kiuchumi kwa kufanya biashara ya ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, kuku wa nyama na ameendesha maisha yake vizuri akitumia mkopo aliokuwa anaupata.

Amesema, anawasihi wanawake wengine wasisite kuchukua mikopo kwani inasaidia kuinua wanawake kiuchumi na pia ACB wamekuwa ni moja ya taasisi wasikivu hususani pale mteja anapokua amekwama.
Mkurugenzi wa Bodi ya Akiba Commercial Bank (ACB)  Rukia Adam akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa tawi la Kijitonyama wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Machi 08 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Bodi ya Akiba Commercial Bank (ACB)  Rukia Adam akizungumzia mkakati waliojiwekea benki hiyo katika kutoa fursa ya ajira kwa wanawake na usawa katika sehemu za kazi kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 08, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Bodi ya Akiba Commercial Bank (ACB)  Rukia Adam akiwa katika picha na wateja wa benki hiyo baada ya kuwapatia  zawadi kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 08, mwaka huu
Salma Rashid Ally mteja wa benki ua Akiba  kwa kipindi cha miaka 20, amewasihi wanawake wengine wasisite kuchukua mikopo kwani inasaidia kuinua wanawake kiuchumi.