Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imefuta safari zake za kwenda nchini Comoro, na hivyo kuifanya iwe imefuta safari zake kwenda kwenye mataifa manne tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona katika mataifa mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kuwa ndege ya ATCL inafanya safari yake ya mwisho hii leo kutoka Dar es salaam kwenda Comoro, na baada ya hapo abiria ambao tayari wamekata tiketi kwa ajili ya safari watarudishiwa fedha zao bila chaji yoyote ya ziada.

Safari nyingine zilizofutwa na ATCL kwenda nje ya nchi ni pamoja na ile ya kwenda Mumbai nchini India baada ya serikali ya nchi hiyo kuzuia wageni kuingia nchini humo hadi Aprili 15 mwaka huu, ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Safari nyingine zilizofutwa na ATCL ni ile ya kutoka Dar es salaam kwenda Entebbe Uganda na ile ya kutoka Dar es salaam kwenda Bujumbura Burundi, sababu ikiwa ni hiyo hiyo ya mlipuko wa virusi vya corona.