MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa jana amecheza kwa dakika zote 90, timu yake, Aston Villa ikiendelea kuvurunda katika Ligi Kuu ya England baada ya kuchapwa 4-0 na wenyej, Leicester City Uwanja wa King Power.

Kipigo kinazidi kuiporomosha Aston Villa inayofundishwa na kocha Muingereza, Dean Smith sasa ikibaki na pointi zake 25 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kukamata nafas ya 19, ikiizidi pointi nne Norwich City inayoshika mkia katika ligi ambayo mwisho wa msimu timu tatu zitateremka daraja.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Michael Oliver, mabao ya Leicester City inayofundishwa na kocha wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers yalifungwa na Harvey Barnes dakika ya 40 na 85 na Jamie Vardy mawili pia, dakika ya 63 kwa penalti na 79.

Kwa ushindi huo, Leicester City inafikisha pointi 53 baada ya kucheza mechi 29 na kuendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya Manchester City yenye pointi 57 za mechi 28 na Liverpool yenye pointi 82 za mechi 29.

Kikosi cha Leicester City kilikuwa; Schmeichel, Pereira, Evans, Soyuncu, Justin, Ndidi/Mendy dk84, Albrighton, Praet/Tielemans, Maddison, Barnes na Iheanacho/Vardy dk60.

Advertisements