NA TIGANYA VINCENT
KAMPUNI ya Tumbaku ya Alliance One Tanzania (AOTTL)  imeukabidhi uongozi wa Mkoa wa Tabora vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 23.9.

Msaada huo umekabidhiwa jana na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni hiyo David Mayunga kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri katika halfa iliyofanyika Ofisini kwake.

Mayunga alivitaja vifaa vilivyotolewa ni Bati 270, Saruji mifuko 300  na nondo 320.

Alisema msaada huo kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na vyoo  katika Wilaya ya Tabora na Wilaya ya Uyui kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike.

Mayunga alisema Wilaya ya Tabora imepewa mifuko 200 ya saruji na nondo 240 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 8.6.

Alisema msaada huo ni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari ya Itojanda na Ndevelwa zote za Manispaa ya Tabora.

Mayunga alisema kwa upande wa Wilaya ya Uyui wamekabidhi mabati 250 , mifuko 100 ya saruji na nondo 80 kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa Mabweni ya watoto wa kike katika Sekondari ya Idete na kumalizia majengo ya shule mpya ya Nsimbo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri aliwataka Idara Wakuu wa Wilaya zote zilizopata msaada huo  kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo ya kutoa mazingira mazuri ya watoto wa kike kupata elimu.

Alionya kuwa hatasitakuchua hatua kwa watendaji wote waliopewa vifaa ambao watavitumia kwa maslahi binafsi.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala aliishukuru Kampuni ya Alliance One kwa msaada huo ambao utawasaidia kuongeza kampeni yake ya kujenga mabweni kwenye shule mbalimbali ili kuwa kinga watoto wa kike na mimba.

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na watoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na huku njiani wakikutana na vishwawishi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya alisema msaada waliopata utasaidia kumalizia mbweni ya wasichana  katika Shule ya Idete ambayo walikuwa washaanza kujenga chini ya Kampeni ya Nishike mkono kuwasaidia watoto wa kike wapate elimu.