Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Magharibi ya Asia (ESCWA) amesema, matokeo hasi ya mripuko wa kirusi cha corona ni ya kutisha.

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Yaumu-Sabi'i, Dakta Rola Dashti amesema: "Tathmini za awali kuhusu matokeo hasi ya mripuko wa kirusi cha corona zinatisha mno, kwa sababu tutapoteza watu wengi, hali ambayo haiwezi kufidika."

Katibu Mtendaji wa ESCWA ameongeza kuwa, ajira nyingi zitapotea kutokana na mripuko wa corona, ambao utasababisha pia hasara ya mabilioni ya dola.

Dakta Dashti amebainisha kwamba, mripuko wa Corona utawafukarisha watu wengi, utawafanya wakimbizi na watu wengi wanaotafuta hifadhi wakose misaada, utazidisha ukatili dhidi ya wanawake na kuifanya hali ya afya iwe mbaya sana.

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, utatuzi wa taathira hasi za mripuko wa kirusi cha corona hautapatikana kwa kuchukuliwa hatua katika maeneo husika tu, bali inapasa itayarishwe mipango katika ngazi za nchi zote duniani.

Idadi ya watu walioambukizwa kirusi cha covid 19 duniani kote hadi sasa imefikia 597,262, ambapo watu 27,365 wamefariki dunia na wengine 133,363 wamepata nafuu.