MACHOZI! Staa wa filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ amemliza upya mama wa aliyekuwa mwigizaji maarufu Bongo, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa baada ya kukiri kuwa alishatoa mimba mbili za mwanaye huyo.

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA baada ya kuulizwa anazungumziaje ishu ya Wema kukiri kuwa aliwahi kutoa mimba mbili za Kanumba, mama huyo alisema alisikia kusisimka nywele kutokana na kauli hiyo na anatamani mno kuonana uso kwa uso na Wema ili wajue watafanya nini.

“Jamani mpaka nywele zilinisisimka kabisa, natamani sana kuongea na Wema nikae naye maana uzuri ni kwamba amekiri mwenyewe kuwa alitoa mimba za mwanangu, yaani imeniumiza sana jamani,” alisema mama Kanumba.

Mama huyo aliongeza kuwa anampenda mno Wema kuliko hata Lulu (ndiye alikuwa mpenzi wa Kanumba kabla ya umauti) kwa sababu ni mtu ambaye anamkumbuka na hata wakikutana popote mrembo huyo anamfurahia mno.

“Natamani sana Wema aje nimuone, nina kitu nataka kumwambia na ninampenda kwa sababu ni binti wa tofauti sana kuliko alivyo Lulu, kwani kila anionapo popote anakuwa na furaha sana na mimi. Natamani Kanumba angekuwepo jamani,” alisema mama Kanumba huku akiwa na kwikwi ya kilio.

Kanumba ambaye alifariki dunia Aprili 7, 2012, enzi za uhai wake aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Wema na ndiye aliyemuingiza kwenye uigizaji ambapo waliachana na baadaye kuingia kwenye uhusiano na msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Stori: Imelda Mtema, Dar