JUMLA ya watu Milioni 3.3 wamefanikiwa kupatiwa huduma za matibabu ya afya bila malipo zinazoendeshwa na benki ya Biashara ya NBC kupitia programu yake ya kliniki zinazohamishika (mobile Clinic).

Huduma hiyo ilianzishwa tangu mwaka 2002 imeweza kutoa matibabu kwa wananchi wa maeneo tofauti nchini.

Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano wa Benki ya Biashara ya NBC, William Kallaghe wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari na Rais John Magufuli kuelekea maadhimisho ya 55 ya siku ya madaktari nchini yanayodhaminiwa na benki hiyo.

Amesema wamekuwa wakitoa huduma hiyo ya bila malipo kwa kinamama na watoto chini ya umri wa miaka mitano na kuongeza kuwa kupitia huduma hiyo kundi hilo limeweza kupata huduma na tiba za magonjwa mbalimbali.

Kalaghe amesema, wanatoa huduma hiyo kupitia kliniki zao zinazohamishika ambazo ni magari yanayopita mitaani katika na kutoa huduma hiyo ya bila malipo kwa kinamama na watoto hao.

"Tumeanza programu hii tangu mwaka 2002 na mpaka sasa tuna jumla ya magari matatu ambayo yapo barabarani yakifanya huduma hiyo nayo jumla ya wagonjwa waliohudumiwa chini ya mpango huo wamefikia Milioni 3.3 ambao wengi wao ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam," amesema.

Aidha ameeleza, sababu kubwa ya yao kudhamini maadhimisho hayo ya miaka 55 ya madaktari nchini, ni kutokana na benki hiyo kuwa wadau wa sekta ya afya kwani wamekuwa wakiunga mkono sekta hiyo hususani katika masuala ya huduma za mama na mtoto.

"Sababu nyingine zilizotufanya tudhamini maadhimisho haya ni umuhimu na mchango wa madaktari katika Taifa letu hivyo sisi tumeona ni vema tushirikiane nao kama wadau wao, japokuwa tunatoka sekta ya kifedha tumeona lazima twende sambasamba na sekta ya afya kwani lengo letu ni moja wao wanaimarisha afya za watanzania na sisi tunahakikisha watanzania wanawezeshwa,"

Hata hivyo amesema benki hiyo imekuwa ikitoa mitaji kwa hospitali binafsi ambao wanamahitaji ya kuagiza mitambo kutoka nje ya nchi kwa kuwapatia mikopo.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati amesema chama hicho kinatimiza miaka 55 tangu kuanzishwa kwake na Machi 4 mwaka huu watakuwa na kambi ya utoaji wa huduma za matibabu bila malipo katika viwanja vya Zakhem Mbagala.

Amesema wakati chama hicho kinaanzishwa kilikuwa na madaktari 23 lakini hivi sasa wamefika zaidi ya 15,000 na kuongeza kuwa kati ya hao kuna madaktari vijana ambao wapo tayari kwenda kufanya kazi mahali popote nchini.
 Askofu wa Kanisa la Mennonite, Dayosisi ya Mashariki na Pwani Askofu Nelson Kisare akielezea jambo kwa kwa Meneja Uhusiano wa Benki ya Kibiashara ya NBC William Kallaghe (wa pili kulia), wengine ni Afisa Masoko Tawi la NBC Samora Dustane Lipawaga (kulia) na Meneja huduma za Jamii Irene Peter (kushoto) wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) yaliyofanyika leo (jana) yakihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
 Meneja uhusiano wa Benki ya Biashara NBC William Kallaghe akizungumza na waandishi wa habari akielezea benki ya NBC inavyotoa mchango wake katika sekta ya afya wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) yaliyofanyika leo (jana) yakihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dr Faustine Ndungulile akipata maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano wa Benki ya biashara ya NBC William Kallaghe (kulia), wengine ni Afisa Masoko Tawi la NBC Samora Dustane Lipawaga (kushoto) na Meneja huduma za Jamii Irene Peter wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) yaliyofanyika leo (jana) yakihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dr Faustine Ndungulile akisalimia na Afisa Masoko Tawi la NBC Samora Dustane Lipawaga akiwa na Meneja Uhusiano wa Benki ya biashara ya NBC William Kallaghe (kulia) na Meneja huduma za Jamii Irene Peterwakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) yaliyofanyika leo (jana) yakihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.