Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umempongeza Mjumbe wa Kudumu na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano Dkt Tobias Lingalangala kwa kutunukiwa shahada ya uzamivu (PHD) kutoka Shirika la LeadImpact ya nchini Marekani.

Lingalangala ametunukiwa shahada ya uzamivu ya Doctorate in humanity baada ya taasisi hiyo kuona juhudi kubwa alizozifanya kwa jamii.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumpongeza, Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Dkt Mshindo Msolla amesema baada ya kupata taarifa kuwa mmoja wa watendaji wa muda mrefu ndani ya Klabu ya amefurahi ametunukiwa shahadu ya uzamivu tena katika masuala ya jamii ambalo ni jambo kubwa sana.

Msolla amesema, uongozi wa Yanga unampongeza sana Dkt Lingalangala kwa hatua kubwa aliyoipiga katika kusaidia jamii na kurudisha mchango wake hadi kufikia hatua ya kutunukiwa shahada hiyo.

"Sisi kama uongozi wa Yanga tunajivunia kuwa na kiongozi kama Dkt Lingalangala kwani amekuwa ni moja ya viongozi wanaojitoa sana nilifikiri ni kwa klabu ya Yanga tu kumbe hadi kwa jamii, amefanya  mambo makubwa sana nasi kama uongozi wa Yanga tunampongeza," Dkt Msolla.

Ameeleza kuwa, Lingalangala ameifanyia makubwa sana Yanga ikiwemo kufanya usajili wa mchezaji mmoja na hasa akiwa kamati ya mashindano ambayo ni nyeti ndani ya klabu yao.

Kwa upande wake Dkt Lingalangala ametoa shukrani kwa uongozi wa Yanga kwa kuendelea kumuamini ndani ya Klabu hiyo kwa kumpatia ujumbe wa kudumu.

Amesema, hakutegemea kupata shahada hiyo kwani hakufahamu kama mchango wake kwa jamii una thamani kubwa sana na ameishukuru Shirika la LeadImpact kwa kumtunuku kitu  chenye thamani kubwa kwenye maisha yake.

Pia, ameishukuru familia yake kwa ujumla kwa kumpasapoti kwa kila jambo analofanya kwa jamii na ana imani kuwa huu ni mwanzo bali ataendelea kujitoa kwa kila atakachokipata.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu mbalimbali, Lingalangala amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa kuendelea kumuamini na amewataka kuwa na subira kwani kwani bado wanaendelea kuijenga timu yao.

Mwishoni mwa wiki hii, Lingangala alikua ni moja ya watunukiwa shahada za uzamivu (Doctorate in Humanity PHD) Kutoka shirika la LeadImpact la nchini Marekani baada ya kujenga mradi mkubwa wa maji kwenye mji wa Njombe pamoja na kutoa elimu ya kilimo na ufugaji wa kisasa kwa wananchi wa mji huo.