KWA sasa muziki wa Bongo Fleva umeshamiri sana, umevuka mipaka ya nchi, bara na unasikilizwa duniani kote.

Lakini hadi Bongo Fleva inafika katika mafanikio haya, kuna watu wengi ambao kwa kiasi kikubwa wamesahaulika na hawatajwi sana, ingawa ni miongoni mwa waliojitoa kwa hali na mali kuhakikisha Bongo Fleva inafikia ilipo sasa.

Hautakosea kama ukisema hawa ndio wenye Bongo Fleva yao, yes! Nimekusogezea orodha ya watu ambao siyo wasanii lakini wana mchango mkubwa sana katika Bongo Fleva:

P FUNK MAJANI

Wengi wanamfahamu kwa jina la P Funk lakini jina halisi ni Paul Matthysse, moja kati ya watayarishaji wahenga wa muziki wa Bongo Fleva lakini pia wenye mchango mkubwa sana uliouweka muziki huu kwenye ramani.

Alianza rasmi kazi ya kutengeneza muziki mwaka 1995 enzi za uchanga wa Bongo Fleva, alipoanzisha studio yake inayojulikana kwa jina la Bongo Records. Alifanikiwa kutengeneza ngoma kali zilizofanya muziki huo kupendwa na kusikilizwa.

Lakini pia alifanikiwa kutengeneza ngoma zilizowapa majina makubwa wasanii wengi. Mfano mzuri ni Juma Nature, Solo Thank, Sister P, AY, Zay B, Mike T lakini pia amewahi kufanya kazi kadhaa na wakali kama Professor Jay, Afande Sele na wengine wengi.

ADAM JUMA

Huyu ni muongozaji video au vichupa vya nyimbo za wasanii aliyeleta mabadiliko makubwa katika muziki wa Bongo Fleva na kampuni yake ya Next Level. Siyo kwamba tunabeza mchango wa waongozaji kama Benchmark Production iliyotengeneza ngoma kadhaa kama Zali la Mentali ya Professor Jay, 2 Eyes Production iliyotengeneza ngoma ya Zeze ya T.I.D, Mwananchi Video, Royal Production, Chapakazi Film na nyingine kadhaa, lakini Adam Juma ndiye muongozaji aliyeleta mabadiliko makubwa katika video za wasanii wa Bongo Fleva. Kazi zake zilikuwa na ubora, jambo lililopelekea kuchezwa katika vituo vikubwa kama Channel O na MTV Base.

RUGE MUTAHABA

Ruge Gelase Mutahaba ama ukipenda unaweza kumuita jasiri muongoza njia, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina.

Ni mmoja kati ya watu waliofanya mapinduzi makubwa katika muziki wa Bongo Fleva. Mwaka 1998 akishirikiana na Joseph Kusaga, walianzisha kituo cha redio ambacho ndio Clouds FM ya leo.

Moja ya maudhui yaliyopewa kipaumbele sana ni muziki huo, ulichezwa sana lakini pia ilitumika kama kipaza sauti cha wasanii wengi kuzungumza mambo mbalimbali kuihusu sanaa hiyo.

Lakini pia mwaka 1999 alianzisha Smooth Vibes ambayo ilikuwa na jukumu la kusaka vipaji na kuviendeleza na hatimaye wakapatikana wasanii wakubwa, miongoni mwa wasanii walioibuliwa hapa ni pamoja na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Rehema Chalamila ‘Ray C’, Abubakar Katwila ‘Q Chief’, Banana Zorro na wengine wengi.

Baadaye akaja na Tanzania House Of Talent, nyumba ya vipaji iliyowaibua wasanii wengi. Lakini pia ni moja ya waasisi wa Tamasha la Fiesta.

SAID FELLA

Huyu naye ni mmoja wa watu wa mwanzoni kabisa kusimamia wasanii, wengine walijifunza mengi kutoka kwake. Shughuli hizi alianza rasmi mwaka 2000, kwanza alitafuta vipaji mtaani lakini pia aliwasimamia kuhakikisha wanautambua muziki kinagaubaga, lakini pia alisimamia utengenezwaji wa kazi zao kuanzia audio hadi video.

Hakuishia hapo, aliwatafutia soko wasanii hao ikiwa ni pamoja na matamasha mbalimbali. Miongoni mwa wasanii waliopita katika mikono ya huyu mtu ni pamoja na Juma Nature, Chege, Temba, Aslay, Mbosso na wengine wengi.

MASTER J

Jina lake halisi ni Joachim Maunde Kimario, ni mtayarishaji wa muziki wa Bongo Fleva. Amefanya makubwa katika kutengeneza kazi mbalimbali zilizofanya vizuri na kusifika sana.

Alianzisha studio yake ya MJ Production mwaka 1996, ni miongoni mwa studio chache za kitambo ambazo mpaka sasa bado ipo.

HITIMISHO

Orodha ya watu walioupiga tafu muziki wa Bongo Fleva ni pana sana kiasi kwamba inatuwia vigumu kumueleza kila mmoja, lakini kwa harakaharaka itoshe kuwataja wengine kama Abubakar Sadiki, Sebastian Maganga, DJ Stive B, Taji Liundi, Miika Mwamba na Bizman Ntavyo.