Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakiwemo viongozi wa Taasisi za Kijamii, Mashirika yasiyo ya kiserikali,waendesha bodaboda,watu wenye ulemavu na viongozi wa dini na kimila wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakipeana mrejesho wa mambo waliyojifunza kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kufanya maamuzi kwa nia ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu ushiriki wa wanawake leo Ijumaa Februari 14,2020 katika ukumbi wa BM Maganzo. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mzee wa Mila Juma Kidaha Makwaiya kutoka kata ya Ukenyenge akitoa mrejesho wa alichojifunza katika mafunzo hayo. Aliitaka jamii kuachana na mila zilizopitwa na wakati na kuhakikisha inawaamini wanawake kuwa viongozi ili kuwa na ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge,Anjelina Mahona akiwataka wanawake kujitambua na kujiamini na kutopenda kuitwa wapiga debe wa wagombea wanaume bali wao wajitokeze kwa wingi kuwania nafasi za uongozi.
Mwenyekiti wa Chama cha waendesha bodaboda kata ya Ukenyenge,Zephania Charles akiwashauri wanawake kujikubali na kujiamini kuwa wanaweza kuwa viongozi na kuacha kubezana wao kwa wao na wanaume kuwashika mkono wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mayanji kata ya Ukenyenge, Sheikh Othman Ndamo ambaye ni Sheikh wa kata ya Kishapu akizungumza wakati wa mafunzo hayo. Alisema wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za uongozi kwani kinachohitajika katika uongozi ni akili,busara na hekima  na hivyo vyote mwanamke anavyo.
Mratibu wa miradi wa Shirika la AGAPE ACP linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto,Peter Amani akishauri wadau kutowaacha nyuma wanaume katika kupigania haki za wanawake na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi.
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii,Costantine Dasse akizungumza wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ualbino wilaya ya Kishapu, Seif Rashid akizungumza wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi. Alisema Watu wenye ualbino wanatamani kuona wanawake wanakuwa viongozi kwani asilimia 99 ya watu wenye ualbino wamelelewa na akina mama baada ya akina baba kutelekeza familia zao. 
Mzee wa Mila Isanzule Nkinga kutoka kijiji cha Mwaweja kata ya Mwaweja akizungumza wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi . Alisema : “Wanawake wakihamasishwa watajitokeza kugombea nafasi za uongoze tuendelee kuwatia moyo na kuwapa elimu wanaume wanaohisi kudharauliwa kama wanawake watakuwa viongozi,tuwaambie kuwa suala la uongozi ni la kila mtu katika dunia ya leo”.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi  wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakitengeneza mpango kazi wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakitengeneza mpango kazi wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakitengeneza mpango kazi wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Mchungaji wa Kanisa la KKKT kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge, Godlisten Mzula akiwasilisha mpango kazi wa kundi lake wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Mwezeshaji Jamii, Genes Tarimo akiwasilisha mpango kazi wa kundi lake wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo akiwasilisha mpango kazi wa kundi lake wakati wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakipiga picha ya pamoja baada ya kumaliza mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi wakipiga picha ya pamoja baada ya kumaliza mafunzo hayo.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog


Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) umeendesha mafunzo ya Jinsia, Demokrasia na Uongozi kwa viongozi wa Taasisi za Kijamii, Mashirika yasiyo ya kiserikali,waendesha bodaboda,watu wenye ulemavu na viongozi wa dini na kimila wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi.

Mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Wanawake na Uongozi unaosimamiwa na TGNP Mtandao kwa ufadhili wa UN Women yamefanyika Februari 12,2020 hadi Februari 14,2020 katika Ukumbi wa BM katika kata ya Maganzo yakishirikisha wadau zaidi ya 40.

Lengo mafunzo hayo ni kuwawezesha wadau hao kupeleka elimu kuhusu masuala ya jinsia,demokrasia na uongozi kwa makundi wanayoyaongoza ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kufanya maamuzi kwa nia ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu ushiriki wa wanawake.

Washiriki wa mafunzo hayo wamesema mila potofu na wanawake kutojiamini bado ni changamoto kubwa inayochangia wanawake wengi kuwa na hofu ya kugombea nafasi za uongozi hivyo wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kuhusu faida za wanawake kuwa viongozi

Aidha wameshauri elimu ya wanawake kujiamini ianze kutolewa katika ngazi ya shule ya msingi ili vijana wakue wakiwa na uelewa na jamii ipewe elimu ya haki za binadamu na usawa na kijinsia.



Mwenyekiti wa kijiji cha Mayanji kata ya Ukenyenge, Sheikh Othman Ndamo ambaye ni Sheikh wa kata ya Kishapu

alisema wanawake wanatakiwa kupewa nafasi za uongozi kwani kinachohitajika katika uongozi ni akili,busara na hekima  na hivyo vyote mwanamke anavyo kwa hiyo ana sifa ya kuwa kiongozi huku akiwashauri wanaume wawape uhuru wa kuamua,kushiriki maamuzi na kumiliki rasilimali.


"Mwanamke ni chuo cha familia na mwanamke ndiyo mwenye kujenga familia hivyo akiwa kiongozi, ndani ya uongozi wa uongozi kunakuwemo huruma,upendo na uadilifu",aliongeza Sheikh Ndamo.

Kwa upande wake, Mzee wa Mila Juma Kidaha Makwaiya kutoka kata ya Ukenyenge aliitaka jamii kuachana na mila zilizopitwa na wakati na kuhakikisha inawaamini wanawake kuwa viongozi ili kuwa na ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi.

“Mwanamke na mwanaume wakiwa pamoja katika ngazi za maamuzi,wakawa na maamuzi shirikishi wanaleta maendeleo chanya.Tusiwachulie wanawake kuwa hawawezi bali tushirikiane nao kwa faida yetu sote”,alisema Makwaiya.

“Zamani wanawake waliothubutu kugombea nafasi za uongozi walionekana kuwa ni wahuni na Malaya na wasio na maadili. Malezi waliyolelewa wakielezwa kuwa wanawake hawawezi kuongoza ndiyo yaliwafanya wawe waoga na wakimya kumbe walikuwa wanajiumiza wenyewe na kujikuta wanakosa haki zao”,alisema Mzee Makwaiya.

Mzee wa Mila Isanzule Nkinga kutoka kijiji cha Mwaweja kata ya Mwaweja alisema : “Wanawake wakihamasishwa watajitokeza kugombea nafasi za uongoze tuendelee kuwatia moyo na kuwapa elimu wanaume wanaohisi kudharauliwa kama wanawake watakuwa viongozi,tuwaambie kuwa suala la uongozi ni la kila mtu katika dunia ya leo”.

Hata hivyo, Mchungaji wa Kanisa la KKKT kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge, Godlisten Mzula alisema ukosefu wa elimu ya uongozi ndiyo changamoto kubwa inayowafanya wanawake washindwe kujiamini hivyo panahitajika jitihada ziendelee kufanyika kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya wanawake.

Mchungaji wa Kanisa la FPCT kata ya Ukenyenge,Silvery Shartieli alishauri jamii ipewe elimu ya kwamba mwanamke ana uhuru wa kugombea na anaweza kuongoza jamii.

“Viongozi wa dini tunakutana na wananchi kila wiki,tuendelee kutoa elimu hii kwani inasikitisha kuona baadhi ya watu kuwabeza wanaume wanaotetea haki za wanawake na kuonekana pengine wana maslahi kwa wanawake hao",alisema.


Mratibu wa miradi wa Shirika la AGAPE ACP linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto,Peter Amani aliwashauri wadau kutowaacha nyuma wanaume katika kupigania haki za wanawake na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi.

“Wakati tunahamasisha wanawake,ni lazima tuzungumze pia na wanaume waone umuhimu wa kutoa nafasi kwa wake zao,watoto washiriki kwenye chaguzi mbalimbali”, alisema Amani.

Mwenyekiti wa Chama cha waendesha bodaboda kata ya Ukenyenge,Zephania Charles aliwashauri wanawake kujikubali na kujiamini kuwa wanaweza kuwa viongozi na kuacha kubezana wao kwa wao na wanaume kuwashika mkono wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi.

Mkurugenzi wa asasi ya Access Facility Tanzania yenye makao makuu yake kata ya Ukenyenge,David Isange alisema baadhi ya wanawake wenye sifa za kuwa viongozi hawana elimu na kipato cha kutosha hivyo kusababisha kutojiamini na kujinyanyapaa kwa hofu ya kuogopa kupambana na wanaume katika masuala ya uongozi.

Katibu wa Kikundi cha VICOBA kata ya Maganzo, Happiness Sang’udi na Katibu wa Kikundi cha VICOBA kata ya Mondo,Martha Abel waliwataka wanawake kuacha kubezana wao kwa wao kutokana chuki binafsi na badala yake washikamane na kujiamini kusimama mbele ya umma.

Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ualbino wilaya ya Kishapu, Seif Rashid alisema Watu wenye ualbino wanatamani kuona wanawake wanakuwa viongozi kwani asilimia 99 ya watu wenye ualbino wamelelewa na akina mama baada ya akina baba kutelekeza familia zao. 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge,Anjelina Mahona aliwataka wanawake kujitambua na kujiamini na kutopenda kuitwa wapiga debe wa wagombea wanaume bali wao wajitokeze kwa wingi kuwania nafasi za uongozi huku akiwashauri wanawake kuwashirikisha waume zao wanapotaka uongozi.

Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo alisema hivi sasa wanawake wengi wameanza kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ambapo sasa baadhi ya wanawake wamefanikiwa kuwa viongozi wa serikali za mitaa na udiwani.

Mila na desturi kandamizi mkoani Shinyanga bado zinatajwa kuwajengea nidhamu ya uoga wanawake na kuwa na hofu ya kugombea nafasi za uongozi kwani jamii inamchukulia mwanamke kuwa hawezi kuongoza.

Mbali na changamoto za kiuchumi,ukosefu wa elimu,pia kazi nyingi za nyumbani zinawafanya wanawake kukosa muda wa kushiriki katika masuala ya uongozi.