Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania Mkoa waTanga (Tawla) Wakili Latifa Mwabondo akitoa elimu kwa wananchi katika Jiji la Tanga kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria
Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania Mkoa waTanga(Tawla) Wakili Latifa Mwabondo akitoa elimu kwa wananchi katika Jiji la Tanga kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Tanga Doris Mangure kushoto akimskiliza mkazi wa Jiji la Tanga wakati wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria eneo la Kongwa Jijini Tanga.
CHAMA cha Wanasheria Wanawake Mkoani Tanga (Tawla) kimeeleza kwamba wanatumia sherehe zao za kuelekea kutimiza miaka 30 ya chama hicho kwa kutoa msaada wa kisheria,elimu na shughuli za kijamii kwa wananchi mbalimbali mkoani hapa kwa kuwafuata kwenye maeneo yao.
Ambapo mpaka sasa wamekwisha kutoa elimu ya masuala ya kisheria kwa watu zaidi ya 200 ikiwemo utoaji wa msaada wa kisheria kwa watu 60.
Hayo yalibainishwa na Mratibu wa Chama hicho mkoani Tanga Wakili Latifa Mwabondo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kwamba wamejipanga kutoa msaada huo wa kisheria kwa jamii nzima.
“Kwa kweli sisi kama Tawla tunaendelea kushirikiana na jamii ya wakazi wa mkoa wa Tanga kuweza kutoa elimu kwa wananchi kwa lengo la kuwasaidia kuondosha changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili hasa za kisheria”Alisema
Alisema kwamba tokea waanza kutoa elimu hiyo kuanzia February 1 mwaka huu mpaka February 7 wamefanikiwa kufika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye viwanja vya Tangamano, vyombo vya habari na shule za Changa na Usagara.
“Lakini pia tumetoa elimu kwenye maeneo ya Kwanjeka kwa kuwafikia wakina mama pamoja na msaada wa kisheria kwenye maeneo ya Kata ya Pongwe, Mzizima na Nguvumali na tunaamini itawabadilisha”Alisema
Kwa mkoa wa Tanga Tawla imekuwa ikitoa msaada wa kisheria ,elimu katika maswala mbalimbali ya kisheria na elimu kwa njia ya mdahalo na vyombo vya habari ili kuiwezesha jamii kuweza kufahamu sheria ,haki na wajibu wao.