Mtangazaji wa zamani wa Star TV, Sauda Mwilima ameeleza kuwa meneja wa kwanza wa Diamond Platinumz, Papaa Misifa alitumia uongo wa hali ya juu kuhakikisha msanii huyo anapewa nafasi ya kutambulisha wimbo wake kwenye kipindi chake.

Sauda ambaye alikuwa akitamba na ‘Bongo Beats’ wakati huo, ameeleza kuwa Papaa Misifa alidai kuwa Diamond ni mdogo wake wa tumbo moja na kwamba amekataa shule akilazimisha kufanya muziki, hivyo amelazimika kuuza gari yake ili amsaidie.

“Alijitambulisha kuwa yeye na Diamond ni ‘baba mmoja na mama mmoja’, na kweli ukimuona Papa Misifa alivyo wakati ule na ukimuona na Diamond unaweza kusema kweli ni ndugu jinsi miili yao inavyoendana,” alisema.

“Akasema ‘sasa dogo hataki kusoma na sisi tuko na mama tu, mama ndio anahangaika halafu ndio mwanaye wa mwisho anampenda sana, na dogo hataki kusoma anapenda muziki tu, sasa mimi hapa unavyoniona nimeamua kuuza kigari changu nilikuwa na ki- corolla tu nimekiuza ili dogo aingie studio arekodi kwa sababu mama anatuangalia sisi makaka na anataka tumsimamie kwa sababu anaonekana ana kipaji,” Sauda alisimulia lipofanya mahojiano na Gangana Info.

Alieleza kuwa baada ya kuondoka, mama yake Papaa Misifa alimpa simu mama Diamond pia akaongea naye kusisitiza. Hata hivyo, Sauda anasema uwezo wa Diamond haukuhitaji nguvu kubwa ya uongo aliotumia meneja huyo, kwakuwa baada ya kuangalia video ya wimbo wake alilazimika kuiangalia mara tatu mfululizo akiwa na mhariri wa picha wa ‘Bongo Beats’, na wakaamua kufanya naye kipindi siku iliyofuata.

Bila shaka wimbo huo ulikuwa ‘Kamwambie’, moja kati ya wimbo bora zaidi uliomtambulisha Diamond, huyu ambaye hivi sasa ana tuzo kubwa za kimataifa na mamilioni ya mashabiki duniani.

Alisema siku ya kurekodi kipindi Diamond alikuja na begi la nguo, wakati kipindi kilihitaji tu kuwa na nguo moja.