Ni siku chache baada ya kuenea video inayomuonesha mtoto ambaye anahitaji mchango wa matibabu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imepiga marufuku kitendo cha kuchangisha michango kwa ajili ya matibabu kwa kuwatumia watoto kwa ajili ya kupata pesa.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed, aliyasema hayo alipofika kumjulia hali mtoto Said Ali Ayoub Hamad anaesumbuliwa na ugonjwa wa kensa ya kichwa katika hospitali kuu ya Manzimmoja.

Alisema ni kosa la jinai kwa mtu yoyote kwenda kinyume na sera ya serikali au kufanya kitendo cha uchangishaji bila ya kupitia wizara ya afya na kupata idhini ya kufanya hivyo.

Aidha alisema serakali haijashindwa kuwapatia matibabu wananchi wake na kufahamu sera ya serikali juu ya utoaji wa matibabu bure bila ya malipo ambayo imeanza topkea mwaka 1984.

Waziri Hamad, alisema serikali pia inalipia gharama za matibabu na vifaa tiba, dawa na kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa miaka yote.

Alisema serikali haijawahi kumchangisha mgonjwa yoyote pesa kwa ajili ya matibabu bali inafanya wenyewe na kuhakikisdha mgonjwa anapata tiba.

Alisisitiza kuwa serikali imetoka shilingi billion 7 hadi bilioni 12.5 kwa ajili ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi na kununua vifaa vya matibabu sambamba kusomesha wataalamu kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora.

Aliwatanabaisha wananchi kuwa katika kipindi cha awamu ya saba nchini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein amehakikisha wagonjwa wote wanaotakiwa kupelekwa nje basi wanapelekwa.

Alisema, kipindi cha mieizi sita kilichopita jumla ya wagonjwa 320 walitakiwa kupelekwa nje kati ya hao 236 walipelekwa Dar-es salam na wagonjwa 26 walipelekwa nchini India.

Hata hivyo alisema hivi karibuni timu ya madaktari kutoka nchini Izrael walikuja Zanzibar kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi wagonjwa wa moyo 360 kati ya hao wagonjwa 63 wanapelekwa nchini humo kwa ajili ya matibabu.

Akizungumzia matibabu ya mtoto Said Ali mkaazi wa Micheweni Pemba anaesumbuliwa na ugonjwa wa kensa ya kichwa, alisema serikali haijashindwa kumtibu mtoto huyo kwani alipelekwa Muhimbili lakini baba mzazi wa mtoto huyo alikataa kufanyiwa mionzi na madaktari hivi sasa walishapanga kumpeleka KSMC Moshi.

Waziri Hamad, alisitishwa na baadhi ya watu ambao hutumia wagonjwa kwa ajili ya kuomba misaada kitendo ambacho ni kosa na kumdhalilisha mtoto kwa kufanya biashara kwani serikali haijashindwa kutibu.

“Mtu yoyote au chombo cha habari ambacho kinataka kufanya hivyo basi ni lazima kwanza kupata ruhusa ya wizara kwani serikali haijashindwa kutoa matibabu kwa wananchi wake,”alisema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi hospitali kuu ya Manzimmoja, Hafidh Sheha Hassan, alisema serikali kupitia wizara hiyo imechukua jitihada za matibabu ya mtoto huyo baada ya kugundulika na ugonjwa huo tokea Agosti mwaka 2019.

Alisema,hospitali ya Manzimmoja inaendelea kuchukua jitihada kuona inampeleka KSMC Moshi kupitia kampeni ya upasuaji wa watoto kuona mtoto huyo nae anaingizwa kwa ajili kufanyiwa upasuaji na kuondoa uvimbe uliokuwepo kichwani.

Nae, Mkurugenzi wa Alfahah Charitable Association Rashid Salum Mohammed, alisema tasisi yao inachangisha michango hiyo kwa ajili ya nia njema kwa kumsadia mtoto huyo kwani ipo kisheria na hivi sasa tayari wameshapata shilingi milioni 6.

Aliwasihi watu wenye tabia ya kuchangisha michango kwa malengo yao binafsi kuacha tabia hiyo na kusimama katika uadilifu utu na ubinaadamu.

Baba mzazi wa mtoto huyo Ali Ayoub, alisema ni miaka mitatu sasa mtoto wake anasumbuliwa na ugonjwa huo na kuiomba serikali kuendelea kumsaidia mtoto wake ili apate kupona haraka.