Tangazo la hivi karibuni la rais wa Sudan kusini Salva Kiir kwamba amepunguza majimbo nchini humo kutoka 32 hadi 10 ni tamko ambalo limepokelewa kwa hisia tofauti ndani na nje ya taifa hilo.

Kiongozi wa upinzani ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani Daktari Riek Machar amekaribisha tanganzo hilo la bwana Kiir na kusema ni hatua muhimu katika mchakato wa kuleta amani ya kudumu katika taifa hilo changa duniani ambalo limezongwa na mapigano ya umwakigaji damu ya wenyewe kwa wenyewe.

Siku ya jumamosi rais Kiir alitangaza kwenye taarifa katika mji mkuu wa Juba kwamba Sudan Kusini imerejelea mfumo wa utawala wa zamani wa majimbo 10 na kuwafuta kazi magavana wote wa majimbo hayo. Alisema hatua hiyo itatoa fursa ya kuundwa kwa serikali ya muungano na hatimaye kumaliza vita vya kikabila ambavyo vimekumba taifa hilo kwa miaka mingi.