Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) imezitahadharisha nchi za Afrika Mashariki dhidi ya uvamizi wa awamu ya pili wa nzige wa jangwani.

Ofisa wa ngazi wa juu wa kituo cha utabiri na usimamizi wa hali ya hewa katika jumuiya ya IGAD Bw. Guleid Artan, amesema nzige wa jangwani wanaweza kuzaliana na kuenea katika miezi ijayo kutokana na hali nzuri ya hewa. Ameongeza kuwa nzige wa jangwani wanaweza kuvamia mashamba na mazao katika msimu wa kilimo kati ya Machi na Mei, hali ambayo itatishia usalama wa chakula.

Waziri wa kilimo wa Uganda Bw. Bright Rwamirama amesema maeneo ya kaskazini mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo yameathiriwa na nzige hao.

Waziri wa kilimo na usalama wa chakula nchini Sudan Kusini Bw. Onyoti Adigo amesema wizara yake inahitaji dola milioni 20 za kimarekani kwa ajili ya kupambana na nzige wa jangwani wanaoingia kutoka kusini mwa jimbo la Ikweta Mashariki.