BAADA ya hivi karibuni habari kuzagaa kuwa msanii wa filamu ambaye alikuwa mlokole, Rose Alphonce ‘Muna’ amebadili dini na kuolewa na mwanaume wa Kiislam, ndoa hiyo imezua utata mkubwa.  Habari za awali zilieleza kuwa Muna aliolewa ndoa ya Kiislam baada ya kubadili dini na kuwa muislam na kupewa jina la Samia ambapo mwanaume aliyemuoa ni Mwarabu ambaye ni mfanyabiashara mkubwa nchini China.

“Unaambiwa Muna aliamua kufunga ndoa hiyo ya kimyakimya japokuwa wambea walinasa picha kuanzia akiwa anapambwa, lakini zile za ndoa akiwa na mumewe ndiyo bado hazijaanza kuvuja, ila ameolewa na mwanaume tajiri ambaye ni Mwarabu anayemiliki makampuni huko China,” kilisema chanzo hicho.

UTATA WAIBUKA

Licha ya picha akiwa amevaa nguo za harusi na kupambwa kama bibi harusi kuzagaa mitandaoni, utata mkubwa umeibuka kwani swali la msingi watu wanauliza mwanaume aliyemuoa yuko wapi.

Swali hilo linakuja kutokana na kila picha inayoonekana yupo Muna peke yake na hakuna hata moja inayomwonyesha akifunga ndoa, kitu ambacho baadhi ya watu wanatafsiri inawezekana siyo ndoa ya kweli bali amefanya kiki.

“Sasa hii ni ndoa gani ambayo hata bwana harusi haonekani, au kajioa mwenyewe? Yaani hawa wasanii wana mambo ya ajabu sana, inawezekana anatuchezea akili zetu. Huwenda anatengeneza muvi au wimbo,” alisema mdau mmoja kwenye mtandao wa Instagram.

Utata mwingine ni kwamba kwenye ndoa hiyo waalikwa hawaonekani, je haikuwa na watu? Pia inawezekana vipi Muna ambaye alikuwa anajinadi kuwa mlokole hasa, kukubali kubadili dini na kuolewa ndoa ya Kiislam.

AJITOA INSTAGRAM

Wakati Ijumaa iliyopita habari zikipamba moto kuwa ndiyo siku anayoolewa, Muna aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba anapumzika mtandaoni huko kwa muda lakini cha kushangaza baada ya siku tatu akarudi na kuweka picha kadhaa akiwa amevaa gauni hilo la harusi.

KIONGOZI WAKE AZUNGUMZA

Akizungumza na Amani, kiongozi wa waimba injili kutoka katika Chama cha Tanzania Music Foundation ‘TAMUFO’, Stella Joel alisema wao wamesikia taarifa hizo japokuwa mwimbaji huyo hakuwaalika, hivyo kama kweli Muna amebadili dini na kufunga ndoa ya Kiislam, ameanguka.

“Kama ni kweli Muna ameolewa na Muislam, ameanguka maana Biblia inasema; msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini kwa upande wa watu waliookoka. Hairuhusiwi kuolewa na mtu ambaye hajaokoka, yaani kumkiri Yesu kama Mwokozi,” alisema Stella.