Mtoto mwenye umri wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Kapset nchini Kenya amekutwa akiwa amejinyonga kwa Kamba kwenye mti baada ya kutuhumiwa kuiba Shilingi 300 (sawa na shilingi 6,800 za Tanzania).

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi nchini humo, mtoto huyo alipotea nyumbani kwao Ijumaa iliyopita baada ya mjomba wake kumtuhumu, na baba yake ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuona akiwa amejinyonga.

Kamanda wa Polisi wa eleo la Kapset, Dalamas Kitur alisema kuwa mtoto huyo alikuwa amegombezwa na mama yake ambaye alimuona akiwa anatoka kwenye nyumba ya mjomba wake kabla Sh. 300 hiyo haijapotea.

Ameongeza kuwa kabla ya tukio hilo, mama yake alikuwa amemkamata akiwa na saa mpya na Sh.100 za Kenya mfukoni mwake.

“Mvulana huyo alikuwa anafirikia kuwa lazima baba yake atamuadhibu vikali, akapotea majira ya jioni na baadaye mwili wake ulipatikana juu ya mti siku iliyofuata asubuhi,” Kitur aliwaambia waandishi wa habari.

Alisema kuwa uchunguzi zaidi kufuatia tukio hilo umeanza haraka baada ya maafisa wa polisi kutembelea sehemu ya tukio.