AMEUMBUKA! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mjengo ambao mke wa msanii wa Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Fahima Msenga ‘Fahyvanny’ kujinadi kuwa wamejenga kwa kudunduliza na mumewe, kubainika kuwa walipanga.

Miezi kadhaa iliyopita kwenye mahojiano na gazeti ndugu na hili; Ijumaa, mrembo huyo alisema nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Salasala, Dar ni mali yao na wamejenga kwa shida yaani kwa fedha za kuokotaokota.

CHANZO CHANENA

Baada ya kutoa maelezo hayo, vyanzo mbalimbali vilivyo karibu na Fahyvanny ambaye ni mwanamitindo, kiliweka wazi kuwa siyo nyumba yake bali wamepanga.

“Hiyo nyumba siyo ya kina Rayvanny bali wamepanga, lakini ndiyo hivyo Fahima amekuwa akijinadi kuwa ni yao. Ngoja tusubiri, ipo siku ukweli utajulikana tu,” kilisema chanzo mara baada ya mwanamitindo huyo kujitapa kwamba ni nyumba yao.

AUMBUKA!

Hivi karibuni katika mtandao wa kijamii wa Instagram, picha ya nyumba hiyo ilisambaa kuwa inapangishwa na watu kujikuta wakihoji kwamba inakuwaje wakati inamilikiwa na Rayvanny na mkewe.

“Haya makubwa jamani, hii nyumba si alikuwa anaishi Rayvanny na mkewe Fahima ambaye alikiri kuwa ni yao wanaimiliki, imekuwaje leo wanaipangisha!” Alihoji mmoja wa wadau mtandaoni humo.

Ili kuujua ukweli juu ya nyumba hiyo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta dalali aliyekuwa akipangisha nyumba hiyo, anayejulikana kwa jina la Dalali Kiongozi, ambapo alisema kuwa ni kweli nyumba hiyo inapangishwa na hiyo ni baada ya Rayvanny kumaliza muda wake.

Alipoulizwa kuhusu mmliki wake ni Rayvanny, dalali huyo alisema siyo kweli, alikuwa ni mpangaji tu na mmiliki halali yupo, ndiyo maana Rayvanny ameondoka na sasa anapangishwa mtu mwingine kwa kodi ya milioni 1.8 kwa mwezi. “Kuhusu Rayvanny kwamba alipewa notice ndiyo maana amehama, siyo kweli bali ameondoka kwa sababu kodi yake iliisha,” alisema dalali huyo.