Mtayarishaji nguli wa Muziki wa Bongo Fleva aliyefanya kazi kwa kipindi cha miaka 25 sasa, Master Jay ambaye ni mmoja kati ya watayarishaji waliozaa aina hiyo ya muziki, amesimulia jinsi alivyofanya kazi kwa bidii hadi kuanguka ghafla na kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Master Jay ambaye alianza kuzalisha nyimbo za Bongo Fleva wakati huo hata aina hiyo ya muziki bado haikuwa na jina, yaani tangu miaka ya 1995, ameeleza kuwa baada ya kufanya kazi kwa nguvu na bidii ya aina yake kwa kipindi cha miaka takribani 13 mfululizo, afya yake iliyumba.

“Unajua mimi niliwahi kuanguka nikapelekwa Afrika Kusini, watu wengi hawajui. Kwa sababu hata afya iliyumba, nilikaa Afrika Kusini kwa miezi mitatu hivi kwa ajili ya matibabu. Miaka 13 ya kufanya kazi huku unalala kwa saa mbili au saa tatu tu kwa siku, sio mchezo,” Master Jay alisimulia kwenye The Playlist ya Times Fm akihojiwa na Lil Ommy na Ammy Gal.

Alisema kuwa akiwa nchini Afrika Kusini alikokaa kwa miezi mitatu, Daktari wake alimueleza kuwa asipobadili aina ya maisha yake anaweza kupotea ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano.

“Daktari aliniambia kuwa ‘usipobadilisha maisha yako na jinsi unavyokula’…, nilikuwa na kilo 10, kwa sababu studio utafanya nini zaidi ya kula tu na kazi. Aliniambia kuwa ‘usipobadili maisha yako miaka mitano ni mingi’…,” alisimulia akiitaja miaka ya 2005/2006 kuwa ndiyo ulikuwa wakati huo.

Alisema baada ya kutoka Afrika Kusini alifanya albamu mbili kubwa, kati ya albam hizo ilikuwa ‘Pamoja na Ndani ya Game’ ambayo iliunganisha wasanii wengi na kazi kubwa, na kisha akaamua kustaafu kazi ya kutayarisha muziki.

Hata hivyo, pamoja na kufanya kazi kwa nguvu akiita ilikuwa wakati wa ‘machozi, jasho na damu’, ujira ulikuwa mdogo kwa kuanza kufanya kazi bure hadi kurekodi wimbo mmoja kwa Shilingi 5,000 tu. Kumbuka hivi sasa wimbo mmoja mkubwa unarekodiwa kwa kati ya Shilingi milioni 1 hadi milioni 3.

Master Jay amekuwa akieleza kuwa Sugu ndiye msanii wa kwanza kumlipa fedha nyingi kwa albam, ambapo alirekodi albam yake ya kwanza kwa Shilingi 50,000. Sio kwamba alikuwa hana uwezo wa kufanya kazi nyingine, Master Jay alikuwa tayari ni msomi mwenye shahada (digrii) ya Uhandisi wa Umeme aliyosomea barani Ulaya, hivyo alikuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingine yoyote na wazazi wake walikuwa wasomi, lakini aliipenda zaidi kazi ya muziki na akahangaika nayo.

Ameeleza kuwa baada ya kurudi na kuchagua kufanya kazi ya utayarishaji wa muziki aliingia kwenye mgogoro mkubwa na baba yake ambaye alieleza kuwa walimsomesha kwa fedha nyingi na nyingine walikopa.

“Mzee [Baba] sikuongea naye miaka mitano, na alikuwa hataki hata kuniona, kwa sababu alisema ‘una digrii, mimi nina ‘connection’ ya kukupatia kazi lakini unafanya haya. Mama yangu alisikitika lakini unajua watoto wa kiume ni watoto wa mama, kwahiyo mama yangu alinisapoti sana,” alisema.

Anasema hata walipoanza kupeleka nyimbo zao redioni wakati huo FM Radio ilikuwa moja tu, walikutana na pingamizi kubwa kutokana na ubora wa kazi zao. Uongozi wa radio hiyo ulipinga wakiweka sharti la kuwasilisha nyimbo kwa mtindo wa CD na sio kaseti kama walivyokuwa wanafanya wao.

“Sasa mimi na P Funk tulienda Marekani kuuliza mtambo wa kuchoma CD wakati huo tukaambiwa ni $5,000 (zaidi ya Milioni 10 za Tanzania),” alisema Master Jay, akieleza kuwa hawakuweza kununua kwakuwa hata kipato kwenye kazi yao ngumu kilikuwa sawa na bure.

Master Jay anaeleza kuwa anakumbuka Master T ndiye aliyefanikiwa ‘kwa mbinde’ kushawishi uongozi wa radio hiyo ya FM kuanza kupiga nyimbo hizo kwa kaseti na alipewa dakika tano tu.

Hata hivyo, dakika tano hizo zilionekana kupokewa kwa nguvu na wasikilizaji, ndipo akangezewe dakika 10, dakika 30, saa moja na zaidi. Baadaye muziki huo ulibatizwa jina la ‘Bongo Fleva’, na sasa kila kitu ni historia na teknolojia imerahisisha kila hatua ya uzalishaji, usambazaji na uimbaji.

Nikukumbushe tu: Master Jay alifanya mahojiano hayo na Lil Ommy na kuweka historia katika uwiano mzuri. Kwanza mahojiano ya kwanza aliyowahi kufanya na mtangazaji huyo akiwa katika kituo kimoja mjini Tabora ndiyo yaliyompa kazi Times Fm; lakini mahojiano haya yaliyofanywa wiki iliyopita na huyo huyo Master Jay yalikuwa ya mwisho kwa Lil Ommy kufanya kazi katika kituo hicho akihamia rasmi kwenye kituo kingine.

Times Fm ndiyo radio ilimtambulisha vizuri zaidi Lil Ommy na kumfanya ashinde Tuzo mbili za Mtangazaji Bora wa Radio/TV barani Afrika.