Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Ruth Msafiri akizungumza wakati akifungua warsha ya wadau wa misitu ili kujadili mikakati jumuishi ya namna ya kupunguza matukio ya moto Nyanda za Juu kusini yaliyofanyika Mkoani Njombe.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri William akichangia mada wakati wa warsha ya kujadili mikakati jumuishi ya kupunguza matukio ya moto.
Mwasilisha mada Prof. John Kessy akieleza namna muongozo wa udhibiti wa masuala ya moto unavyotakiwa kufanya kazi na hatimaye kuweka mikakati madhubuti katika maeneo ya vijiji na jamii kwa ujumla
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Ruth Msafiri (mstari wa kwanza, wa .
wanne toka kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya  wadau wa misitu kutoka Nyanda za Juu Kusini.

Wananchi watakiwa kutambua thamani ya mazao ya misitu kwa kuondokana na matumizi ya moto yasiyokuwa sahihi

Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Ruth Msafiri amewataka wadau wa mazao ya misitu kutambua thamani ya misitu na kuonyesha ushirikiano katika kupambana na matukio ya moto misituni.

Ameyasema hayo leo tarehe 10 Februari,2020 wakati alipokuwa akifungua warsha ya siku mbili ya wadau wa misitu Nyanda za Juu Kusini iliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) iliyofanyika katika ukumbi wa Njombe Mji uliopo katika Mkoani Njombe .

Hata hivyo amewasisitiza wadau kuwa na mipango madhubuti katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na uwepo wa sheria ndogondogo ambazo zitawalazimu wananchi kuzifuata kwaajili ya kuondoa majanga ya moto ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.

Akimkaribisha Mgeni aliyekuwa Mwenyekiti wa warsha Bw. Bakari Mohamed ambaye ni Afisa Misitu Kutoka TFS amesema kuwa lengo la warsha hii ni kuendelea kukumbushana juu ya kupambana majanga ya moto ya misituni na namna ya ushiriki wa wananchi pindi majanga haya yanapojitokeza.

Bw. Bakari ameongeza kuwa ni vyema kutambua changamoto zilizopo ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kujua vyanzo,athari zilizojitokeza na namna ya kukabiliana nazo na jinsi ya kuungana katika kupambana na majanga ya moto.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri William amesema kuwa suala la matumizi sahihi ya moto liwekewe mikakati madhubuti ikiwemo ni sambamba na utoaji wa taarifa za matukio ya moto kwa wakati na sheria zilizowekwa za uanzishaji wa moto kusimamiwa na viongozi wa maeneo husika.

Aidha wadau wameendelea kuweka msisitizo katika suala la utoaji elimu kwa jamii lipewe kipaumbele hasa katika msimu wa kiangazi ambao umekuwa na matukio mengi ya moto.

Warsha hii itaendelea kesho tarehe 11 Februari 2020 ikiwa lengo kuu ni kupanga mikakati endelevu ya udhibiti wa moto wa misituni ambapo mafunzo hayo yamejumuisha wadau kutoka katika taasisi mbalimbali zinazojihusisha na mazao ya misitu Nyada za Juu Kusini.