Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
 KAZI inayofanywa na Askari Polisi wa Amani nchini Congo kutoka Arusha- Tanzania Ally Babu ya kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili na vivutio vya Utalii  vilivyopo nchini Tanzania, imeweza kuleta matokeo chanya.

Hilo limekuja baada ya watalii kutokea nchini congo wanaofanya kazi Umoja wa Mataifa kuja nchini kwaajili ya utalii.

Essam Ghoneim raia mwenye asili ya Misri mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Congo amekuwa mtalii wa kwanza kufika nchini Tanzania akiwa na mwenzake kuja kutembelea vivutio vya utalii.

Ikumbukwe kuwa, Watalii hao wameweza kufika nchini baada ya kupata ush meawishi kutoka kwa askari polisi anaeshiriki ulinzi wa Amani nchini Congo Ally Babu.

Watalii hao wamewasili nchini Februari 18 mwaka huu, na kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii na kuahidi kurejea tena.

Watalii hao waliwasili na kuelekea katika mji wa Kilimanjaro na baadae Arusha wakifurahi kufika nchini Tanzania na kuahidi kuendelea kurudi kwa utalii Zaidi katika maeneo mengine ya nchi wapatapo likizo.

Aidha katika ukuzaji wa Kiswahili baadhi ya askari kutoka nchi mbali mbali duniani wanaojifunza kiswahili kupitia Ally Babu wameanza kuelewa na kuongea kiswahili.

Ally Babu ambaye pia ni mwanasheria  amekuwa akijitolea kutangaza utalii na kufundisha walinzi wa Amani wenzake wa umoja wa mataifa lugha ya Kiswahili katika muda wake wa ziada baada ya majukumu yake ya kazi. 

Haya ni matunda ya uzalendo wa kitanzania kukuza na kutangaza lugha adhimu ya Kiswahili na vivutio vinavyopatikana nchini Tanzania.
 Essam Ghoneim (kushoto)  raia mwenye asili ya Misri mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa Nchini akiwa na rafiki yake baada ya kufika nchini Tanzania kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii katika Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha.
Picha ya Mlima Kilimanjaro iliyopigwa na Essam Ghoneim baada ya kutembelea kivutio hicho.