Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. Imani Sichwale akionyesha tangazo lililoamuru kufungwa kwa eneo la uuzwaji wa mazao ya mifugo ambalo lilipuuzwa.
Baadhi ya vifaa vinavyo tumika katika kukata na kusafishia mazao ya mifugo.

Baadhi ya uchafu wa kwato uliotupwa kiholela katika eneo maarufu kwa uuzwaji wa mazao ya mifugo katika Manispaa ya Morogoro.
Muonekano wa eneo la uuzwaji wa mazao ya mifugo kama miguu vichwa na mkia.
Mapipa yanayotumika kuchemshia mazao ya mifugo.

Na Agrey Evarist, Morogoro.

Bodi ya nyama nchini yafungia eneo linalotumika kama mauzio ya mazao ya mifugo katika Manispaa ya Morogoro na kutoa onyo kali kwa watakao endelea kufanya shughuli hiyo.

Bodi hiyo ya nyama iliyokua ikiongozwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. Imani Sichwale wamefika katika eneo maarufu kwa kuuza mazao ya mifugo kama miguu ya n'gombe (kongoro), mikia sambamba na vichwa lililopo karibu na machinjio ya nyama ya Morogoro ambapo akabainisha eneo hilo si rasmi na wakaamua kulifunga ili kutoendelea kwa biashara hiyo.

Akielezea sababu za kufunga eneo hilo Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. Imani Sichwale ameeleza serikali ilishapiga marufuku uuzaji wa nyama maeneo ya wazi kwakuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea magonjwa ya mlipuko kama kipindu pindu kutokana na inzi kuruka hovyo hivyo si vyema biashara hii kufanyika kiholela.

"Kuna kanuni na sheria ya nyama ya 10 ya mwaka 2006 inayojieleza wazi na kupinga uuzaji wa nyama katika maeneo ya wazi'' amesema kaimu huyo, hata hivyo anabainisha tayari walisha mwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro juu ya kufungwa kwa eneo hilo na kubainisha kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa likisababisha wananchi kulishwa nyama ya wanyama ambao tayari wamekufa (vibudu) kutokana na kutokua na usimamizi wa kutosha kukagua nyama inayouzwa katika eneo hilo.

''Mkoa wa Morogoro umekuwa na wizi mkubwa wa mifugo na wezi wa mifugo wengi wamekuwa wakijificha katika eneo hili kwa kuchinja nyama kiholela za wizi porini na kuja kuuzia katika maeneo haya hivyo kufungwa kwake kutapunguza wizi wa mifugo mkoani hapa'', amesema Bw. Sichwale.

Kwa upande wake Daktari wa mifugo wa Manispaa ya Morogoro Peter Lema akabainisha soko hilo limekuwa kero kwa muda mrefu na tayari walishamwandikia barua mmiliki wa eneo hilo bila mafanikio hivyo wanaipongeza bodi ya nyama kwa kuweka nguvu katika swala hilo.

Nao wafanyabiashara wa nyama katika eneo hilo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Abedi Makonya wameeleza eneo hilo kwa muda wamekuwa wakifanya biashara zao bila matatizo huku wakieleza wanachouza si nyama bali ni mazao ya nyama ambayo si rahisi kuuziwa buchani.

''Unakuta unaenda buchani kununua nyama lakini unataka na mkia au kongoro, buchani huwezi washa moto ukaanza kwangua miguu ndio maana huwa tunakuja kuchomea huku hivyo serikali inapofanya maamuzi yake iangalie na watu kama sisi", amesema Mwenyekiti Makonya.

Aidha mjasiriamali Latifa Ramadhani anayejusisha na mama lishe amebainisha wao wanaendesha maisha yao kwa kutumia eneo hilo kununua baadhi ya mazao hayo ya mifugo kama utumbo kupika na kuuza chakula hivyo nao wakaiomba serikali kuandaa eneo lingine kwaajili ya kufanyia shughuli zao.