Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof Kitila Mkumbo (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja( wa pili kulia) wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji uliohusisha ujenzi wa Vituo vya kusukumia maji na matenki matano ya kuhifadhia maji.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
WAZIRI wa Maji Prof Makame Mbarawa  ameziunganisha Mamlaka ya Maji na  Usafi wa Mazingira  Chalinze (CHALIWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanzia Januari 11, 2020.

Maamuzi hayo yanapelekea Waziri  kuvunja bodi ya Chaliwasa na kuanzia sasa itakuwa na kuwa chini ya bodi ya Dawasa inayoongozwa na Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange.

Hatua hiyo Imefikiwa baada ya mamlaka ya Chaliwasa kushindwa kujiendesha kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof Kitila Mkumbo amesema maamuzi hayo yamefanywa na Wizara kutokana na Chaliwasa kushindwa kujiendesha ikiwemo kununua umeme na kuendeleza miradi iliyopo.

Amesema, hivi karibuni Dawasa walikabidhi miji ya  Mkuranga na Kisarawe na tayari miradi inaendelea na Kisarawe imeshakamilika wakijenga kwa fedha za ndani kutoka kwenye mapato wanayoyakusanya kila mwezi  na kwa upande wa Chalinze kuna mradi wa Chalinze Mboga wanaujenga pia.

Kitila amesema, serikali inakusanya takribani bilioni 23 kwa mwezi kutoka Mamlaka zote, na Dawasa wanakusanya nusu ya makusanyo hayo na tayari walikuwa wanawasaidia Chalinze katika kujenga miradi na hata kuwapatia dawa.

“Chalinze wana changamoto kubwa mbili, gharama za uendeshaji ikiwemo kununua umeme na madawa hivyo Dawasa ni mamlaka ina uwezo wa kujiendesha kutokana na mapato wanayokusanya kwa mwezi, na tumeona ni vizuri tukiwakabidhi rasmi mji wa Chalinze uwe chini yao ili wasimamie vizuri,”amesema Mkumbo.

Mkumbo amewapongeza Dawasa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa uhakika na huduma zikiendelea kuboresha sambamba na kupelekea maji kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya maji kwa kipindi kirefu.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof Kitila Mkumbo akinawa maji kutoka kwa wateja waliounganishiwa huduma hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tenki kuhifadhia maji  la Salasala na kituo cha kusukumia maji.