Na Mwandishi wetu Mihambwe.
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ameagiza kukamatwa mara moja kwa Wazazi wanaowazuia ama kutokuwapeleka Watoto wao shule wale ambao wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza.
Gavana Shilatu ameyasema hayo wakati akizungumza na Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mweminaki iliyopo kata ya Kitama wakati wa ziara yake ya kutembelea shule zote za Sekondari zilizopo Tarafa ya Mihambwe ambapo hakuridhishwa na kiwango cha kuripoti shuleni kwa Wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza.
"Nazungumza nanyi Wanafunzi ambao mnawajua Wanafunzi wenzenu waliofaulu kidato cha kwanza na wapo nyumbani. Nendeni mkawaambie Wazazi wao watakaokaidi kuwapeleka shuleni Watoto wao Serikali itatumia vyombo vyake kuwakamata wote. Usalama wao wawalete Watoto shule mara moja." Alisema Gavana Shilatu
Akizungumza na Mwandishi wetu mara baada ya ziara hiyo Gavana Shilatu alisema sababu wanazotoa Wazazi za kushindwa kuwapeleka Watoto shule hazina mashiko ni za kuishi kwa mazoea kutokana na mwamko mdogo uliopo licha ya Serikali kutoa Elimu bure.
"Mwaka jana walisema hawana hela hata ya kununua sare za shule kutokana na malipo ya Korosho kuchelewa, mwaka huu wamelipwa fedha za Korosho kwa wakati lakini bado hawawapeleki Watoto shule, hapa tatizo si fedha. Sasa mwendo ni ule ule tutawakamata wote wasiowaleta Watoto shule." Alisisita Gavana Shilatu.