Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika ziara yake ya kikazi, mkoani Singida.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Bw.Rashid Mandoa akijibu hoja za watumishi wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mkoani Singida.
Baadhi ya watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) katika ziara yake ya kikazi mkoanI Singida.
Mlinzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Bw.Joseph Ghaba akiwasilisha malalamiko yake wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mkoani Singida.

Na Happiness Shayo, Singida

Watumishi wa Umma nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kufanikisha juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kukuza uchumi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika ziara ya kikazi mkoani Singida.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa ni lazima watumishi wa umma waheshimu kazi na wahakikishe wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo kwa kuwa Serikali ya Awamu ya tano haitovumilia watumishi wazembe.

“Mtumishi wa Umma ni tunu kwa hiyo ni bora ukachezea mshahara kuliko kuchezea kazi kwa sababu wapo wanaotamani kuingia serikalini lakini hawana fursa hiyo” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Dkt. Mwanjelwa ametoa wito kwa Watumishi wa Umma nchini kufanya kazi kwa kuendana na spidi ya Mheshimishimi Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na si kwa kulegalega.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya uadilifu, utendaji kazi uliotukuka , haki na haiko tayari kumuonea mtumishi yeyote.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Watumishi wa Umma kuwa na subira katika kipindi ambacho serikali inafanyia kazi changamoto zao za malimbikizo ya mishahara, kupandishwa madaraja na nyinginezo.

Mhe.Dkt. Mwanjelwa yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Singida kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na kukutana na Watumishi kwa lengo la kusikiliza maoni na kutatua kero zao.