Mwenyeketi wa bodi ya Taasisi CAMFED Jeanne Ndyetabura (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari, namna taasisi hiyo inavyoshirikiana na serikali katika kuboresha mazingira rafiki kielimu nchini kwa watoto wa kike, hayo yamezungumzwa leo wakati wa mkutano uliofanyika katika makao makuu ya shirika hilo, jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa taasisi ya CAMFED Tanzania, Lydia Wilbard
Mkurugenzi wa taasisi ya CAMFED Tanzania, Lydia Wilbard (kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano uliofanyika leo katika makao makuu ya shirika hilo, jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mwenyeketi wa bodi ya Taasisi CAMFED, Jeanne Ndyetabura.
Mkurugenzi wa Taasisi ya CAMFED TANZANIA, Lydia Wilbard (watatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanufaika wa Taasisi hio pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo.
Taasisi ya CAMFED inayojishughulisha na uboreshaji wa mazingira sambamba na kupiga vita unyanyasaji wa watoto wa kike waishio katika mazingira magumu, inatarajia kuwanufaisha wanafunzi wa kike wapatao 9877 kupitia program wezeshi ikiwemo utoaji wa vifaa vya shule kama Sare, madaftari na chakula.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu (27, Januari 2020) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Lydia Wilbard amesema kuwa dunia ikiwa imesherehekea siku ya elimu duniani, tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2005 imetoa msaada wa vifaa, semina na chakula kwa wasichana wapatao elfu 50 katika kugharimia ada, pesa ya mitihani na gharama nyinginezo kabla serikali haijapitisha mpango wa Elimu bure nchini.
Amesema kuwa taasisi ya CAMFED inafanya kazi kwa kushirikiana na serikali kupitia wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI pamoja na Ustawi wa jamii katika kuandaa makongamano na warsha mbalimbali zenye lengo la kuwajengea wasichana uwezo wa kujisimamia na kutambua haki zao.
Shule takribani 471 zimenufaika mpaka sasa kupitia taasisi hiyo kutoka mikoa ya Shinyanga, Tabora, Mwanza na Mara. Aidha ameitaka serikali kuweka nguvu zaidi katika kuondoa vikwazo na changamoto mbalimbali kwa mtoto wa kike ili kupunguza utoro, mimba za utotoni na kukatikiza masomo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya CAMFED, Jeanne Ndyetabura amesema kuwa ndani ya msichana kuna jamii hivyo CAMFED inawasaidia watoto wa kike ili kuijenga jamii bora ya baadae.
Amewataka wazazi na jamii kutolaumu utoro wa watoto wa kike bali ifuatilie sababu za utoro huo ambazo amezitaja kuwa ni pamoja na vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi, ukosefu wa vifaa na unyanyasaji wa kijinsia.
CAMFED kupitia mtandao wake wa (CAMA) ulioanzishwa mwaka 2014 imekuwa ikiwajengea watoto uwezo wa kujiamini kupitia waandaa mafunzo ambao wamezifikia shule zipatazo 471 mpaka sasa.
Pia taasisi hiyo ina mpango wa kukuza wigo mpana wa utoaji huduma na msaada katika maeneo mbalimbali nchini ambayo hayajafikiwa na huduma hizo hasa watoto wa kike.