Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sleiman akitoa ripoti ya robo ya pili ya utekelezaji wa majukumu ya kazi katika Wizara ya Afya kwa Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar huko katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja .
Katibu wa Kamati ya Ustawi wa Jamiii ya Baraza la Wawakilishi Mwanaisha Mohamed Kheir akitoa ripoti ya majumuisho ya ziara ya kutembelea vituo vya afya kwa Unguja na Pemba huko katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja .
Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Afya wakisikiliza majumuisho ya Ziara ya kutembelea Vituo vya Afya vya Unguja na Pemba iliyotolewa na katibu wa Kamati ya Ustawi wa Jamiii ya Baraza la Wawakilishi Mwanaisha Mohamed Kheir ( hayupo pichan)i huko katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja .

Na Mwashungi Tahir Maelezo 

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amesema kumebainika kuwepo kwa wagonjwa wa Maradhi ya Malaria ambao wameripotiwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja baadhi ya Vituo vya afya Unguja na Pemba.

Akitoa Ripoti ya robo ya pili ya utekelezaji kwa Kamati ya Ustawi wa huduma za Jamii ya Baraza la Wawakilishi huko katika ukumbi wa Wizara ya Afya amesema wagonjwa waliobainika na malaria walipatiwa matibabu stahiki kwa mujibu wa muongozo uliopo.

Amesema katika kipindi ambacho uchunguzi uliofanyika na kugundulika vimelea vya Malaria kwa wagonjwa waliofika hospitali na Vituo vya Afya ambapo vigae 5,176 (Unguja – 2,820 na Pemba 2,356) vilichunguzwa,Kati ya hivyo, vigae 30 (Unguja- 19 na Pemba 11) ambavyo ni sawa na asilimia 0.6 vilikutwa na vimelea vya Malaria.

Aidha,matokeo ya uhakiki wa vimelea vya malaria yameonesha kuwa asilimia 93 ya walioripotiwa kuwa na ugonjwa huo, na asilimia100 hawana vimelea vya malaria.

Aidha amesema zoezi la ufuatiliaji majumbani kwa wagonjwa walioonekana na vimelea hivyo lilifanyika, ambapo jumla ya wagonjwa 986 (88%) waliogunduliwa kuwa na malaria.

Pia amesema Asilimia 10 ya utekelezaji na ufuatiliaji wa wagonjwa majumbani imeongezeka ukilinganisha na kipindi cha miezi mitatu iliyopita cha Julai – Septemba 2019 ambapo Mafanikio haya yametokana na kuwepo kwa mashirikiano ya kutosha kati ya jamii na wahudumu wa afya.

Hivyo katika hatua nyengine za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa malaria Zanzibar, Wizara kupitia Kitengo cha Kumaliza Malaria Zanzibar inafuatilia sehemu zinazoripotiwa kutoa wagonjwa kwa kufanya uchunguzi yakinifu katika mazalio ya mbu ili kuzuwia maambukizi mapya.

Jumla ya mbu 40 wenye vimelea vya malaria wamekamatwa katika maeneo ya Kibokwa na Fungurefu kwa Unguja na mbu 20 wamekamatwa kwenye maeneo ya Fundo, Tumbe na Bopwe kwa Pemba, na vilevile ufuatiliaji wa mazalio ya mbu katika ngazi ya Wilaya zote zimepatiwa viuatilifu kwa mujibu wa mahitaji.

“Mikutano saba (7) ya kuhamasisha jamii ilifanyika katika ngazi tofauti kwa Unguja na Pemba. Mada kuu zililenga juu ya zoezi endelevu la ugawaji vyandarua pamoja na upatikanaji na utoaji wa elimu ya afya juu ya ongezeko la ugonjwa wa Malaria katika shehia za Kisiwandui,Kisima-majongoo, Kikwajuni Bondeni na Kikwajuni juu katika wilaya ya Mjini” , alisema Naibu Waziri.

Akielezea kwenye Huduma Shirikishi za Ukimwi, Homa ya Ini,Kifua Kikuu na Ukoma huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU ziliendelea katika vituo vyote vinavyotoa huduma hizo. Katika kipindi cha robo mwaka ya pili, watu 56,770 (43,286 Unguja na 13,484 Pemba)walichunguzwa VVU katika vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU nakupatiwa huduma za mikoba (outreach services).

Alisema kati yao, watu 373 sawa na asilimia 0.7 ( 339 Unguja na 33 Pemba) waligunduliwa na VVU. Aidha, hadi kufikia Disemba 2019, jumla ya watu 6,710 wanaoishi na VVU wanapatiwa huduma na tiba kwenye kliniki 13 (Unguja 9 na Pemba 4).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Mwanasha Khamis Juma akitoa majumuisho ya Kamati ya Ustawi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa Wizara ya Afya amesema kamati ilitekeleza majukumu yake kwa kutembelea katika vituo vya afya kwa Unguja na Pemba.

Alisema kwa upande wa Pemba alitembelea baadhi ya vitengo vya Wizara ya Afya pamoja na kupata maelezo ya miradi hiyo inavyoendelea na miongoni mwa Hospitali walizotembelea ni Hospitali ya Vitongoji na kubaini kwamba sehemu ya kuhifadhia dawa ni ndogo na kupelekea dawa nyengine kukosa sehemu nzuri ya hifadhi.

Akitoa mchango mjumbe wa kamat hiyo ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Fuoni Yussuf Hassan Idi amesema Wizara ya Afya imeweza kupata mafanikio makubwa katika sehemu mbali mbali za Hospital na matarajio zaidi yataweza kupatikana hatua kwa hatua.