Sehemu ya Wananchi wa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam wakiwa wamempanga msururu katika kituo cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kilichopo Kawe, kwa ajili ya kuwasajili ili aweze kukamilisha mchakato wa kusajili laini ya simu ya mkononi kwa kuweka alama za vidole. Picha na Avila Kakingo, Globu ya Jamii.
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.
MISURURU mirefu ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaaam imeonekana kwenye vituo mbalimbali ambavyo vimewekwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa ajili ya kuwasajili wananchi ikiwa ni mchakato wa kuhakikisha kila mwenye laini ya simu ya mkononi anaisaijili kwa kuweka alama za vidole.
Katika maeneo kadhaa ya uandikishaji wa vitambulisho vya NIDA watu wameonekana kujitokeza mapema kuanzia saa 12 asubuhi ili kuhakikisha wanakamilisha utaratibu wa kupata vitambulisho au namba ya NIDA ambayo ndio muhimu zaidi kwenye usajili wa laini za simu.
Wakati wananchi wakiwa wamefurika maeneo ya kupata vitambulisho hivyo, NIDA na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamekuwa wakishirikiana kwa karibu kuhakikisha mchakato huo unakwenda kwa kasi inayotakiwa.Pia RITA ambao wanahusika na utoaji wa cheti cha kuzaliwa na kifo nao wameamua kupiga kambi kwenye maeneo hayo ili wenye uhitaji wa vyeti vya kuzaliwa wanavipata kwa wakati.
Pamoja na hayo yote, Rais Dk.John Magufuli amekuwa akizungumzia mchakato huo na mara kadhaa alikuwa akitoa maagizo kwa mamlaka zinahusika kusogeza mbele muda wa usajili ili Watanzania wengi waweze kusajiliwa na mara ya mwisho alitoa maagizo mwisho utakuwa Januari 20 mwaka na ndio siku ambayo simu ambazo hazijasajiliwa laini zake zitazimwa.
Hivyo iwapo maagizo ya Rais yatabaki kama yalivyo siku za kuzimwa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole siku zake zinahesabika na kuanzia leo zimebaki siku tatu .
Wengine wakihakiki majina yao kwenye ubao uliowekwa kituoni hapo.
Wakizungumza na Michuzi Globu ya jamii leo Januari 18,mwaka 2020, baadhi ya wananchi kwenye maeneo ya uandikishaji wa vitambulisho vya NlDA wametoa maoni tofauti huku wengi wakieleza kuwa kwa sasa wanasubiri huruma ya Serikali kama wataongeza tena muda kwani kwa siku zilizobakia kuna kila dalili laini zao za simu kuzimwa kwani pamoja na baadhi yao kukamilisha hatua zote namba ya NIDA ndio itawachelewesha maana wanatakiwa kusubiri kwa wiki mbili.
Moja ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye naye anapambana kupata kitambulisho cha NIDA katika kituo cha NIDA maeneo ya Kivukoni Posta Mpya David Msumba John amesema amefika kituoni hapo leo saa moja asubuhi na amefanikiwa kukamilisha mchakato saa nane mchana.Hata hivyo hajafanikiwa kupata kitambulisho kutokana na kuelezwa kuwa atapaswa kukisubiri kuanzia sasa hadi Februari 11 mwaka huu.
"Kwa kweli tunasubiri hatma ya Serikali maana idadi ya watu ni kubwa, kwangu nashukuru niseme tu angalau nimefika hatua nzuri naona dalili ya kukipata ingawa nitapewa namba za NIDA wiki mbili kuanzia leo,"amesema Msumba.
Kuna wale walifanikiwa kupata, hivyo huwadolishia ambao bado wanasota kwenye foleni kama ionekanavyo pichani.
Mkazi mwingine Juma Mgogo wa Ukonga jijini, amesema wanatambua dhamira ya Serikali ya kuhakikisha laini zinazajiliwa lakini kwa hali ilivyo anaona muda uliotolewa huenda usitoshe."Nimekuja jana na nikatakiwa kuja tena leo, nimefika mapema sana na hadi muda huu wa saa tisa bado sijafanikiwa ,hata hivyo naamini nitakipata lakini hofu yangu sijajua itakuwa lini."
Kwa upande wake Said Kimoso wa Kimara jijini Dar es Salaam ametoa ombi kwa Serikali kuongeza muda ili Watanzania ambao bado hawajafanikiwa kupata vitambulisho vya NIDA wavipate."Tunaomba Serikali iongeze muda ingawa sijui kama itakubali maana Rais ametoa maagizo mara nyingi ya kuongeza muda,hivyo sijui kama ataongeza tena ingawa tunamuamini kwani siku zote amekuwa na watu wa chini."
Hata hivyo mamlaka zinazohusika zenyewe zimeendelea na majukumu yake ya kuandikisha wananchi ambao bado hawajapata vitambulisho hivyo.
Wengine wakiendelea kupiga soga huku wakisubiria foleni isogee.