MZAZI mwenziye na msanii Nasibu Abdul “Diamond au Mondi”, Tanasha Donna amesema haishi kwa kumtegemea mtu.  Tanasha alikiambia chombo kimoja cha habari nchini Kenya hivi karibuni ambako ndiko alikozaliwa kwamba ana uwezo wa kuendesha maisha yake bila kumtegemea Mondi.

“Wengi wanaamini kuwa mimi ni mtu mwenye tamaa, siyo kweli, ninachojua ni kwamba sijawa tajiri lakini natafuta kipato kupitia nguvu zangu, watu walio karibu yangu wanajua,” alisema Tanasha. Aliongeza kuwa, alipoanza uhusiano wa kimapenzi na Diamond wengi waliamini kuwa amefuata fedha na kwamba yupo kwenye uhusiano kwa ajili ya maslahi jambo ambalo alikana kuliwazia wakati wowote.

Mwanadada huyo ambaye alianza uhusiano na Mondi mwishoni mwa mwaka jana, akichukua nafasi ya penzi la Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, raia wa Uganda ambaye naye alizaa na Mondi watoto wawili, ni mtangazaji wa kituo kimoja cha redio nchini Kenya.

Mbali na utangazaji Tanasha ambaye wazazi wake wana asili mbili; Mkenya na Mwitaliano, pia amekuwa mwanamitindo kwa kipindi kirefu.

Aidha, Tanasha ambaye anaweza kuzungumza lugha tano ambazo ni Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kiholanzi na Kihispania pia ni mwigizaji na mwanamuziki na mwaka jana aliachia wimbo wake matata uliokwenda kwa jina la Radio aliomshirikisha Barak Jacuzzi na pengine kazi hizo ndizo zimekuwa zikimuingizia kipato ambacho anakitambia.