UONGOZI wa Singida United iliyo chini ya Kocha Mkuu, Ramadhan Nswanzurimo umesema kuwa hauna mashaka na mchezo wao wa kesho, Januari 22 dhidi ya Yanga utakaochezwa Uwanja wa Namfua, Singida.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga amesema kuwa wanatambua mchezo utakuwa mgumu ila wamejipanga kupata ushindi.

“Tunatambua Yanga ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu ila hilo halitupi mashaka tupo tayari kuona namna gani tutashinda.

“Mashabiki wajitokeze kutupa sapoti kwani timu imekuwa ikipita kwenye wakati mgumu ila kwa sasa tumeanza kurejea kwenye ubora,” amesema.

Sanga amesema kuwa historia inawabeba kuwa Yanga hawajawahi kupata ushindi katika uwanja wa Namfua tangu wapande Ligi Kuu hivyo wana imani kuwa wataibuka na ushindi na kuendeleza kuwapa maumivu washabiki wa Yanga.

Yanga iliyochini ya kocha mpya kutoka Ubelgiji Luc Eymael,tangu achukue mikoba ya Charles Mkwasa haijapata ushindi huku ikiwa imepoteza mechi mbili mfululizo wakifungwa na Kagera Sugar 3-0 na kupoteza dhidi ya Azam Fc 1-0 mechi zote zilichezwa jijini Dar es Salaam.

Huku Singida United wakiwa nafasi ya 16 ina pointi 10 imeshinda mechi mbili pekee katika mechi 16 ilizocheza mpaka sasa.