Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akizungumza na Wafanyakazi wa Hoteli za Impala na Naura alipokuwa akitatua migogoro ya wafanyakazi hao dhidi ya mwajiri wao.
Sehemu ya Wafanyakazi wa Hoteli za Impala na Naura wakifuatilia maelezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (hayupo pichani).
Mkuu wa Wilaya wa Arusha Mhe. Gabriel Daqaro akieleza jambo wakati wa kikao hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (katikati) akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya wa Arusha Mhe. Gabriel Daqaro (kulia) mara baada ya kutatua mgogoro wa Wafanyakazi wa Hoteli za Impala na Naura dhidi ya Mwajiri wao.

PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

Na; Mwandishi Wetu

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameingilia kati mgogoro wa kazi kati ya wafanyakazi wa Hoteli za Impala na Naura dhidi ya mwajiri wao kufuatia malalamiko ambayo yaliwasilishwa katika ofisi ya Idara ya Kazi Makao Makuu.

Hayo yamejiri Mkoani Arusha Januari 10, 2020 ambapo Naibu Waziri Mavunde alipokea malalamiko mbalimbali ikiwa kutokulipwa mishahara kwa muda miezi zaidi ya sita pamoja na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Kazi.

“Kama mwaajiri unapaswa kufuata sheria na miongozo ya ajira mahala pa kazi ili kila mfanyakazi aweze kupata haki yake, kwa kutekeleza hayo wote mtanufaika na kuwa na mahusiano mazuri kati ya mwajiri na waajiriwa bila matatizo yoyote,” alisema Mavunde

Mheshimiwa Mavunde ambaye aliongozana na Kamishna wa Kazi Kanali Francis Mbindi mara baada ya kusikiliza pande zote mbili alitoa maagizo yafuatayo;

Jambo la kwanza, alitaka ifikapo tarehe 31.03.2020 Wafanyakazi kulipwa mishahara yao yote kwa miezi yote waliyofanya kazi kama ambavyo Mwajiri ameahidi kimaandishi, ambapo January 31,2020 Mwajiri anapaswa kutanguliza mishahara ya miezi miwili kabla hajamaliza kulipa miezi yote iliyobaki.

Suala la pili Kamishna wa Kazi kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi katika Hotel hizo hasa malipo ya ziada na likizo.

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kumfikisha Mwajiri mahakamani mara moja kwa kushindwa kuwasilisha makato ya michango ya Wafanyakazi kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii ilijali wafanyakazi hao kukatwa katika mishahara yao.

Pia, Mashauri yote dhidi ya mwajiri yaliyopo mahakamani hayapaswi kuingiliwa mpaka yatakapoamuriwa, isipokuwa kama kuna nafasi ya kujadiliana nje ya mahakama ni vyema ikatumiwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Naye Mkuu wa Wilaya wa Arusha Mhe. Gabriel Daqaro amewashukuru wafanyakazi hao kwa uvumilivu mkubwa na kufuata utaratibu wa kuwasilisha madai yao na kuahidi kushirikiana na Ofisi ya Kazi Mkoa kuhakikisha maagizo yaliyotolewa yanatekelezeka.

Kwa Upande wake. Mkurugenzi Mtendaji wa Hotel za Impala na Naura Bw. Randy Mrema amekiri kuwepo na mapungufu makubwa katika utekelezaji wa sheria za kazi na kuahidi kurekebisha kasoro zote ambazo zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na changamoto ya ukata wa fedha na kuahidi kuja na mkakati wa upatikanaji wa fedha ndani ya kipindi kifupi kunusuru hali ya wafanyakazi na kuboresha huduma za Hotel hizo amabazo zilijizolea umaarufu mkubwa enzi za uhai wa Mzee Faustine Mrema ambaye alikuwa mmiliki wake kabla mauti hayajamfika.