Luteni Kanali David Luoga wa Kikosi cha Ujenzi cha JWTZ akiwaonesha Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamin Sitta, Kaimu Mkurugenzi Mahudu Kazi, mchoro wa uwanja wa mpira wa miguu utakavyokuwa. Mwenye shati la kijani kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Ndg. Harod Maruma.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sitta katikati akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mahudu Kazi wa kwanza kulia, Luteni Kanali David Luoga wakipitia na kusaini nyaraka za mkataba wa ujenzi wa Jengo la Utawala pamoja na Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sitta mwenyesuti akipeana mkono na Luteni Kanali David Luoga wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mara baada ya kusaini mkataba na ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya Jengo la Utawala pamoja na Uwanja wa mpira wa miguu.

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leo imtiliana saini mkataba na Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa wa kisasa wa mpira wa miguu pamoja na Jengo la kisasa la Utawala la Halmashauri hiyo.

Mkataba huo umesainiwa leo na Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Mhe. Benjamini Sitta pamoja na Luteni Kanali David Michael Luoga na kushuhudiwa na watendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kinondoni Harold Maruma.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Mhe. Meya Sitta amesema kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala utagarimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 huku ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu ukigarimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.7.

Amefafanua kuwa uamuzi wa kutumia JWTZ umetokana na kufuata ushauri unaotolewa kila mara na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kutumia wanajeshi kwa njia ya Force Account kutekeleza miradi ya ujenzi kwa weledi na kwa muda tarajiwa.

Mhe. Meya amesema kuwa miradi hiyo mikubwa miwili iliyosainiwa leo itajengwa na Jeshi la Wananchi kwa kuwa wanaamini watafanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa na wa haraka kulingana na mkataba huo ulivyoeleza.

“ Tunamshukuru Mhe. Rais wetu mpendwa, Dk. Magufuli kwa kutuonyesha njia ya kufanya kazi kwa kutumia wanajeshi kwa kuwa miradi hii itakamilika kwa wakati. Hapa nia kazi tu, hakuna michakato. Miradi hii mikubwa itafanywa na JWTZ” amesema Meya Sitta.

Aidha Mhe. Meya Sitta amesema “ tunampongeza Mkurugenzi wetu Aron Kagurumjuli, kwa kweli tuna mkurugenzi makini, msikivu ,ambaye anafuata maelekezo na ni mchapakazi ndio maana leo Kinondoni yetu ipo hapa” ameongeza.

Kwa upande wake Luteni Kanali Luoga ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kuwaamini kufanya kazi hiyo na kuahidi kukalimisha ujenzi huo kwa muda wa miezi sita.

Luteni Luoga amesema katika ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu, awamu ya kwanza itakamilika kwa kipindi cha miezi mitatu na nusu na awamu ya pili itatumia miezi miwili na nusu.

Ameongeza kuwa katika ujenzi huo, licha ya kwamba Jeshi la Wananchi litafanyakazi hiyo,lakini pia litatoa fursa za ajira kwa watu wengine ikiwemo Mama ntilie pamoja na vijana wengine lengo likiwa ni kila mwananchi apate kipato.

“ Tunampongeza Mhe. Meya Sitta, Mkurugenzi Kagurumjuli kwa kutuamini. Na sisi tunawahakikishia kuwa Jengo la utawala pamoja na uwanja tutakamilisha kwa kipindi cha miezi sita kama ilivyo kwenye mkataba wetu”amesema Luteni Kanali Luoga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma amefafanua kuwa ujenzi huo wa miradi mikubwa miwili iliyotiwa saini leo ni utekelezaji wa ilani CCM.

Imetolewa na Kitengo Cha Habari na Uhusiano 
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.