MUNGU yupo! Hata wale ambao bado wana shaka juu ya hilo, niaminini mimi. Mungu yupo na kupitia maisha yetu hapa duniani, tunaziona ishara za makuu yake sema wakati mwingine tunajisahaulisha tu kutokana na ugumu wa mioyo yetu.

 

Safari ya maisha ya muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ inatosha kuona ukuu wa Mungu na namna ambavyo mwanadamu anatakiwa kujitayarisha na mitihani. Mungu akisema ni wakati wa kupata mtihani, mwanadamu huwezi kupinga.

 

Mipango ya Mungu sio sawa na mipango yetu. Lulu akiwa angali binti mdogo, alianza kuzichanga karata zake kwenye eneo la uigizaji. Kakutana na waigizaji ambao wakati huo walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye, wakaanza kumkuza kisanaa.

 

Bahati nzuri nyota yake ilikuwa njema eneo hilo licha ya umri wake kuwa mdogo, Watanzania walimkubali. Walimpa thamani ya kuwa staa mwenye umri mdogo. Kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote, ni vigumu kidogo kuhimiri kishindo cha ujana, Lulu naye alipitia mapito mengi ya ujana.

 

Alikuwa mtu wa viwanja. Alikuwa binti wa matukio. Kunywa kulewa, kucheza kihasara kwake haikuwa ishu. Vyombo vya habari hususan Global Publishers viliripoti sana matukio yake ya ujana.

 

Wakati huo walikuwepo mastaa wakubwa kiumri kama vile Vincent Kigosi ‘Ray’, Jacob Steven ‘JB’ na wengineo lakini Lulu naye alikuwa miongoni mwao. Kwenye maisha hayo ya ujana, Lulu alijikuta ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na marehemu Steven Kanumba.

 

Kanumba ambaye alikuwa mkubwa kiumri kulinganisha na Lulu. Wakati huo, ilikuwa si rahisi sana kuamini kwamba Lulu anaweza kutembea na Kanumba. Kanumba alikuwa mkubwa kwa umri na hata kiumbo.

 

Wakitembea walikuwa kama mtu na mdogo wake, hivyo ilikuwa si rahisi kuhisi au kufikiria kwamba wawili hao wanaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi. Lakini yote kwa yote, Lulu alihimiri vishindo. Alitembea na Kanumba akiwa angali hajatimiza miaka 18.

 

Waliishi kwenye uhusiano wa siri kwa muda mrefu mpaka pale kifo kilipolidhihirisha penzi lao. Baada ya Kanumba kufariki ndipo kila mtu akajua kwamba Lulu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba. Tena kifo hicho kikampa mtihani binti huyo mdogo.

 

Lulu ambaye uwezo wake wa kiakili ukiwa bado mdogo, alihusishwa na kifo cha Kanumba. Akayaonja mateso yasiyoendana na umri wake. Alishtakiwa kwa mauaji, baadaye ikawa mauaji ya bila kukusudia. Safari za mahakamani zikawa ndio maisha yake.

 

Anatokea gerezani kuelekea mahakamani. Kwa mara ya kwanza anayaonja maisha ya kupigwa picha mahakamani kama mtuhumiwa wa mauaji. Hili si jambo dogo. Kwa kumtazama mwenzako akiwa anaelekea kizimbani, unaweza kuona ni jambo dogo lakini kiuhalisia ni jambo zito sana.

 

Wazazi wa Lulu kipindi hicho walikuwa kwenye majonzi. Kwa vyovyote vile, walikuwa hata wakitamani warudishe siku nyuma na Lulu pengine awe hajajiingiza kwenye uhusiano na Kanumba. Lakini wapi, uhalisia ni kwamba Kanumba alishakufa na Jamhuri ikaendelea na kesi yake.

 

Lulu alipokata rufaa katika kesi hiyo na kubadilishiwa mashtaka ya kuua bila kukusudia, alipata dhamana. Akarudi uraiani kwa miaka kadhaa. Furaha ikaanza kurejea, akaanza kuyafurahia maisha ya uraiani na kujichanganya na watu.

 

Lakini furaha yake haikudumu sana kwani kesi iliendelea, akiwa ameshaanza na kuigiza tamthiliya, ghafla akahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Ndugu zake nao wakarudi kwenye huzuni kubwa. Akatupwa gerezani.

 

Mungu si Athumani, baada ya safari ndefu yenye milima na mabonde, Lulu alikuja kutoka kwa msamaha wa rais. Huo ndio ulikuwa mwisho wa mateso marefu. Akarudi uraiani. Bahati nzuri alishakutana na mchumba wa ndoto yake Majizo.

 

Majizo alikuwa mvumilivu katika kipindi chote cha majonzi ya Lulu. Alipotoka kwa msamaha wa rais, akamvalisha pete na sasa kinachosubiriwa ni ndoa tu.

 

Kimsingi maisha ya binti huyu yanatufundisha kwamba, alipangalo Mungu binadamu hatuwezi kulipangua. Kwenye maisha kuna furaha na majonzi hivyo ni vizuri kama mwanadamu kujiandaa na yote. Nyakati za shida na zile za furaha uzipokee!

Makala: Erick Evarist