Kocha Luc Emayel raia wa Ubelgiji aliyewahi kufundisha klabu mbalimbali za Soka Barani Afrika ametangazwa kuja kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera aliyefungashiwa virago na uongozi wa Klabu ya Yanga.

Kocha huyo mwenye wasifu wa Leseni ya UEFA Pro aliyoipata mwaka 2009, ameshawasili visiwani Zanzibar akiwa ameongoza na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Wadhamini wa Yanga GSM Eng, Hersi Said.

Taarifa ya kuwasili kwa Kocha Emayel imetolewa na klabu ya Yanga kupitia  ukurasa wake wa  Instagram na kuweka bayana muda atakaowasili Kocha huyo mpya katika Uwanja wa Ndege wa Visiwani Zanzibar leo tayari kuungana na timu hiyo iliyopo kwneye mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Yanga  ilivunja benchi zima la ufundi  na kuwapa kibarua kipya Kaimu Kocha Charles Boniface Mkwasa akisaidia na Said Maulidi ambapo kwa sasa kwenye mmashindano ya Kombe la Mapinduzi timu iko chini ya Kocha msaidizi Said Maulid.

Awali kocha huyo ameonekana kufundisha timu mbalimbali nchini Afrika ikiwemo As Vital Club ya nchini Congo DR mwaka 2010 kufanikisha timu hiyo kuchukua Kombe la Super Coupe Du Congo 2011 na raundi ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika na rekodi ya kucheza mechi 23 bila kufungwa.

2011, alijiunga na timu ya Missile ya Gabon kama Kocha  Mkuu na aliisaidia timu hiyo kushinda taji lao la ligi la kwanza katika historia yao ma timu hiyo kufika raundi ya 16 ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penati dhidi yabJS Kabylie.

Timu zingine alizowahi kufundisha ni pamoja na AFC Leopard ya Kenya 2013, Rayon Sports Rwanda 2014/15, JS Kairouan 2015,  Al Nasr 2016 , Al Merrikh 2016/17, Polokwame City 2017/18, Free State Star 2018/19 na Black Leopard 2019.

Kocha Emayel atakuwa jukwaani kuitazama timu yake ikishuka dimbani kucheza mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa majira ya sa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amani Zanzibar.