Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa kushoto,akimsikiliza jana meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira(Mbiuwasa)mji wa Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Patrick Ndunguru wakati Waziri Mbarawa alipotembelea ujenzi wa mradi wa maji katika mtaa wa Kihaha kata ya Lusonga unaojengwa na Mbiuwasa kwa gharama ya shilingi milioni 500 zilizotolewa na wizara hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

SERIKALI imeipatia  Mamlaka ya maji safi na Uhifadhi wa Mazingira mji wa Mbinga(MBIUWASA)  shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa  maji  unaotarajia kuwanufaisha  wakazi zaidi ya 1000  wa mtaa wa  Kihaha kata ya Lusonga Halmashauri ya mji Mbinga  mkoani Ruvuma.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Uhifadhi wa mazingira mji wa Mbinga(MBIUWASA) Mhandisi Patrick Ndunguru alisema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa.

Alisema,mji wa Mbinga unakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 54,896 kati ya hao wakazi 27,572  wanaishi katika maeneo yanayopitiwa na mtandao wa Bomba la maji ambao ni sawa na asilimia 50.2 ya idadi ya wateja waliounganishiwa maji 2893.

Aidha Ndunguru alimweleza Waziri Mbarawa kuwa, kwa  sasa uzalishaji wa maji katika mji wa Mbinga kwa siku ni wastani wa mita za ujazo 3000 ambao ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya maji ambayo ni mita za ujazo 5490 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vitano vikiwa na uwezo wa mita za ujazo 3000 wakati wa kiangazi na mita 4343 wakati wa masika.

Alisema, mradi wa maji wa Kihaha ni mwendelezo wa uboreshaji wa huduma ya maji katika mji wa Mbinga unaotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano  ambao utagharimu shilingi ml 500 hadi kukamilika kwake.

Alisema, katika kuhakikisha wananchi wananufaika na mradi wa maji mwaka wa fedha 2016/2017  MBIUWASA iliweza kujenga tenki la kuhifadhia maji lenye ukubwa wa mita za ujazo 2000 katika kijiji cha Mhekala na ulazaji wa Bomba kuuu la usambazaji maji umbali wa km 1 eneo la Masumuni.

Aidha katika kuhakikisha wananchi wa Mbinga wanapata maji safi na salama katika Mwaka wa fedha 2017/2018 MBIUWASA iliendeleza vyanzo  vya maji vine katika kijiji cha Tukuzi ikijumuisha ujenzi wa miundombinu  mbalimbali ya maji ikiwemo uchimbaji wa mtaro wenye urefu wa km 23.

Alisema, mradi huu wa uboreshaji wa huduma ya maji katika mji wa Mbinga unahusisha kubadilisha bomba za usambazaji zilizo chakaa lengo likiwa ni kukabiliana na upote vu mkubwa wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wateja.

Kwa mujibu wa Ngunguru,mradi huu unatekelezwa kwa utaraibu wa lipa kutokana na matokeo(Force Account)ukisimamiwa na  wataalam kutoka Mamlaka ya maji safi  na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(SOUWASA)kwa kushirikiana na Mbiuwasa kwa kazi ya uchimbaji mitaro  inayofanywa na jeshi la Magereza kupitia gereza la mahabusu Mbinga na ufungaji wa mabomba unaofanywa na Mbiuwasa .

Alisema, mradi huu ulianza kujengwa tangu Mwezi Novemba 2019 ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 75 na unatarajia kukamilika ifikapo Februari mwaka huu.

Ndunguru ameiomba Serikali kufikiria maeneo mengine ya mji wa Mbinga ambayo yameendelezwa lakini hadi sasa kuna uhaba mkubwa wa maji na kuna wakazi wapatao 10150 na taasisi 13.

Kutokana na idadi kubwa ya wakazi katika maeneo hayo, kusambazwa kwa huduma ya maji kutaweza kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika mji wa Mbinga kutoka asilimia 50.2 ya sasa  na kufikia asilimia 90 hata hivyo makisio halisi ya gharama ya mradi  huo shilingi bilioni 1.4.

Naye waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa ameIpongeza  Mbiuwasa kwa kusimamia vizuri miradi ya maji  kwa kufanya kazi kubwa na uadilifu mkubwa wa fedha za Serikali zinazoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika mji wa Mbinga.

Waziri Mbarawa pia ameomba Mbiuwassa kuhakikisha inawatumia wataalam wa ndani kujenga matenki ya maji badala ya wakandarasi ambao wengi wao ni wezi na wabadhilifu wa fedha za miradi ya maji.