Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Iringa, Yusuph Kamotta akionyesha baadhi ya vitu ambavyo havitakiwi kwenye bajaji na jinsi gani madereva bajaji wanavyokiuka sheria za barabarani.

NA FREDY MGUNDA, IRINGA

BAADA ya mgomo wa daladala uliotokea hivi karibuni mkoani Iringa jeshi la polisi limeendesha oparesheni kali na kuwakamata madereva bajaji zaidi ya 25 kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Akizungumza na blog hii, Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Iringa, Yusuph Kamotta alisema kuwa zoezi hilo la kuwakamata madereva bajaji wanaokiuka sheria za usalama barabarani limetokana na migomo midogo ya madereva daladala inayotokea kutokana na mgongano wa kimaslahi hali inasababishwa na madereva bajaji kuingia katika barabara wasizoruhusiwa.

Alisema kuwa zoezi hilo linafanywa na jeshi la polisi baada ya changamoto kubwa kutokea katika barabara kuu ya Iringa kuelekea Dodoma ambapo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na mwingiliano ambao bajaji wanatumia na kuleta mgongano dhidi ya daladala kutokana na kugombea abiria hali ambayo inajitokeza mara kwa mara.

Kamotta alisema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na kuwataka madereva wote wa bajaji na daladala kufata sheria ambazo wamekuwa wakitoa mara kwa mara madereva hili kuondokana na hali ya migomo ya mara kwa mara inayoweza kutokea kwa sababu ya mwingiliano.

“Ndugu mwanabahari tumekuwa tunatoa mara kwa mara elimu kwa madereva wote sisi kama sisi lakini pia kupitia viongozi wao lakini kuna baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani na hao ndio chanzo kikubwa hivyo zoezi hili limefanyika na kuwakamata zaidi ya 25 ambao lazima wafikishwe mahakamani” alisema

Alisema kuwa kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani kwa madereva hao jeshi la polisi linawashikilia na wanapelekwa mahakamani na kuwataka kufata sheria bila shurti kwani jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kiko imara na zoezi litafanyika kila siku hadi kuondoa migomo isiyokuwa ya lazima inayosababishwa na wachache.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Daladala mkoa wa Iringa, Ambakisye Mwangomba alisema kuwa wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya bajaji kufanya kazi ambazo kama daladala wakati biashara yao inatakiwa kukodiwa na zaidi wamekuwa na kondokta kama wapiga debe.

Alisema kuwa baada ya madereva kugoma hivi karibu tulikaa meza moja na kamanda wa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani na kuangalia changamoto hizo za bajaji zinatatuliwa vipi kitu ambacho kimefanyiwa kazi na kuona bajaji zinazokiuka sheria zikichukuliwa hatua na kufanya hali ya usafiri kuwa salama.

“Leo tumeona jitihada za mkuu wa kikosi cha usalama barabarani namna ambavyo anafanya kazi na hali ya usafiri imekuwa shwari kwani wale bajaji wanaokiuka sheria wanakamatwa wao na vyombo vyao na natoa wito kwa jeshi kuendelea kufanya oparesheni ili kuwabaini wanaokiuka sheria hizo” alisema

Alisema kuna baadhi ya madereva wa bajaji wanavunja sheria kwa makusudi licha ya elimu wanayopewa na hii inaweza kuwa ni udogo wa adhabu wanazopewa hivyo kuna umuhimu wa kuongezewa adhabu na kufikishwa mahakamani kuweza kuondoa kabisa wavunja sheria.

Alisema kuwa changamoto kubwa iko katika suala la bajaji kupitia njia ambazo daladala zinapita hasa kwenye njia kuu ambazo wao hawaruhusiwi kupita na kufanya biashara kama ambavyo daladala wanafanya hali ambayo inasababisha madereva daladala wasifanye biashara na kuwapa wakati mgumu kufikisha kiwango walichopangiwa na wamiliki wa daladala.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha Bajaji manispaa ya Iringa, Melabu Kihwele alisema kuwa operasheni inayoendelea inatokana na madereva bajaji kupita katika barabara ambazo hawaruhusiwi hivyo kuvunja makubaliano yaliyowekwa walipoketi pamoja, bajaji daladala, Sumatra, mkuu wa wilaya na jeshi la usalama barabarani na kufikia mwafaka wa daladala wananjia na zao na bajaji wananjia zao.

“Madereva bajaji wamekuwa wanakiuka sheria kwa makusudi kutokana na tayari walishapewa elimu mara kwa mara na hata sisi viongozi tumekuwa tukiendelea kuwaelimisha kuhusu kufata sheria za barabarani lakini bado wamekuwa wakikiuka sheria hizo na hali inayopelekea jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kuwakamata na kuwafikisha mahakamani”alisema.