Msanii mkongwe wa BongoFleva Q Chief, ameiambia Planet Bongo ya East Africa Radio kuwa TID amemuomba msamaha wa kumaliza bifu lao lililodumu kwa miaka minne.


Q Chief amesema TID ame-miss kuwa karibu na yeye ila alishangaa sana jinsi alivyomuomba msamaha, maana alikuwa wa tofauti na siku zote anavyomjua.

"Kitu kimoja ambacho TID anamiss ni kuwa karibu na mimi maana imepita miaka minne ya bifu letu ila watu wategemee vitu tofauti, halafu sitakagi kumzungumzia ila juzi ameniomba radhi, na uombaji wake umenishangaza maana mimi ni mwinyi nataka upole, ila kitu ambacho nilimwambia bifu zuri ni lile linaloisha na kuleta faida" amesema Q Chief.

Wawili hao waliwahi kuwa pamoja katika kundi la Top Band, ambalo lilifanya vizuri kipindi cha nyuma, ambapo kwa mara ya kwanza tangu bifu lao lilipoanza, wameonekana wakiwa pamoja katika Birthday Party ya Shilole iliyofanyika mwishoni mwa mwaka 2019.