Na Abubakari Akida, MOHA
Katika kukabiliana na Matendo ya Udhalilishaji,Ubakaji na Ulawiti Visiwani Zanzibar, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeunda mkakati maalumu lengo ikiwa ni kukomesha matendo hayo ambayo yameota mizizi visiwani humo huku wengi wa waathirika wa matendo hayo wakitajwa kuwa ni watoto wadogo hali inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Akizungumza katika Ukumbi wa Polisi Madema baada ya Kikao cha Ndani na Maafisa wa Juu wa Jeshi la Polisi Visiwani humo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema zinahitajika juhudi za makusudi ili kuweza kukomesha vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya wazanzibar na watanzania kwa ujumla
“Jumla ya kesi 280 zimeripotiwa hapa tu Mkoa wa Mjini Magharibi na tatizo hili linaendelea kukua kwa kasi na inasikitisha sana, jambo hili linachafeua heshima ya nchi yetu, sasa serikali tunakuja na mkakati maalumu ikiwa ni dhamana tuliyopewa kama viongozi,tumeamua kuja na mkakati maalumu na wa kipekee wa kupambana na changamoto ya udhalilishaji,ubakaji na tunaomba mamlaka nyingine zituunge mkono katika mkakati huu sisi kama wizara kupitia Jeshi la Polisi tunaamini mapambano haya hatuwezi kufanya peke yetu..” alisema Masauni
“...pia tunaunda kikosi kazi maalumu ambacho kitaratibu mkakati huo huku kikisimamia uandaaji mafunzo kwa askari wetu hasa wapelelezi wa makosa ya udhalilishaji,kufuatilia kesi zote zilizoenda mahakamani na kuhakikisha zinaenda vizuri hatua kwa hatua,kuhakikisha kesi za udhalilishaji zinapewa kipaumbele badala ya kesi hizo kuchukua muda mrefu hali inayopelekea waathirika wa matendo hayo kukata tama na tunataka kikosi kazi hicho kiwe kiungo na mamlaka nyingine zinazoshughulika na kesi hizo.” Aliongeza Masauni
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Mohamed Hassani Haji anaweka wazi Utekelezaji wa Mkakati huo ambao ni maagizo toka serikalini huku akikiri tatizo hilo la Ubakaji,Udhalilishaji na Ulawiti kukua kwa kasi Visiwani Zanzibar huku akikwaonya wazazi kufika polisi na kuripoti pindi watoto wao wanavyofanyiwa vitendo hivyo.
“Sisi kama jeshi la polisi tnaenda kuunda kikosi kazi hicho,na leo tumepitia majalada hapa na kuona kesi nyingi zimekwama,kwahiyo kikosi kazi hicho kitaanza kazi ndani ya mwezi huu na tunatoa onyo kwa wale wote wanaoshiriki,kusaidia au kuficha matendo haya ya udhalilishaji waache mara moja kwani hakutakua na kuchekeana” alisema Kamishna Hassani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa visiwa hivyo wameiomba serikali kupeleka elimu juu ya kupambana na udhalilishaji mashuleni ambako watoto wamekua wakirubuniwa na vitu mbalimbali ambavyo vimewapelekea kutumbukia katika matendo ya udhalilishaji ambayo yamekua na madhara makubwa Visiwani Zanzibar huku wakiasa kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya wazazi wanaowatetea watuhumiwa na kuyamaliza masuala hayo kifamilia kwani hilo upelekea matendo hayo kuendelea kuota mizizi katika jamii.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiongoza Kikao Maalumu na Viongozi wa Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar, ambapo kikao hicho kiliazimia kuanzishwa kwa Mkakati Maalumu wenye lengo la kupambana na Matendo ya Udhalilishaji, Ubakaji na Ulawiti visiwani humo ambapo waathirka wakubwa wa vitendo hivyo wakitajwa ni watoto huku jumla ya Kesi 280 zikiwa zimeripotiwa ndani ya mwaka huu kwa Mkoa wa Mjini Magharibi pekee.Kikao hicho kimefanyika Ofisi za Kituo cha Polisi Madema,Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi