Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii (wa pili kulia) akiwa pamoja na baadhi ya wakuu wa wilaya kutoka wilaya nane wakijaribu kuruka juu sana kwenye eneo la ”jumping stone” katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato. Eneo hili ni eneo lenye mvuto sana kwa watalii, Aliyeruka juu sana upande wa kushoto wa kwanza ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa, Deogratias Ndejembi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ( wa nne kulia) jana akiwa na Wakuu wa wilaya kutoka wilaya nane nchini wakila chakula kwenye hema pembezoni mwa Ziwa Burigi katika eneo la Mkonje mara baada ya kutembelea sehemu mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Taifa ya BurigiChato mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na na Wakuu wa wilaya nane kutoka sehemu mbalimbali nchini nara baada ya kuwasili katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato akiwaelezea kuhusu umuhimu wa kuhamasisha wananchi wanaowaongoza kutembelea vivutio vya utalii.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Constantine Kanyasu akisalimiana na Afisa Utalii mara baada ya kuwasili na wakuu wa wilaya nane kufika kwa ajili ya kutembelea vivutio vya Utalii.Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Hifadhi hiyo, Damian Salu.
Mkuu wa Hifadhi ya Burigi Chato, Damian Saru akizungungumza na Wakuu wa wilaya kuhusiana na ukubwa wa Hifadhi hiyo huku wakiwa anawasomea ramani jinsi Hifadhi hiyo ilivyo ya kipekee kwa kuwa na wantamapori wa kila aina.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea sehemu mbalimbali katika Hifadhi ya Burigi Chato. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Gairo, Mhe. Siriel Mchembe.
Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza mkakati wa kuwatumia Wakuu wa wilaya nchini kuhamasisha utalii wa ndani.
Kufuatia hali hiyo jana Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe .Constantine Kanyasu aliongozana na Wakuu wa wilaya nane kutoka wilaya mbalimbali nchini kwa ajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya BurigiChato iliyopo mkoani Kagera ili waweze kutambua fursa zinazopatikana ndani ya Hifadhi hiyo mpya.
Mbali ya kutambua fursa hizo, Wakuu wa wilaya hao watatumika pia kuhamasisha wananchi wanaowaongoza katika wilaya watokazo kuhamasisha Utalii wa ndani.
Mhe. Kanyasu amesema Sekta ya Utalii ni sekta muhimu sana katika maendeleo ya nchi hivyo Wakuu wa wilaya zote nchini wapatao 139 ni kundi muhimu katika kuwahamasisha wananchi wanaowangoza kuhusu umuhimu wa kutembelea Hifadhi zilizopo nchini.
Akizungumzia sababu za kuwatumia Wakuu wa wilaya hao, Naibu Waziri Mhe.Kanyasu amesema mbali ya kuwatumia Waandishi wa Habari pamoja Wasanii na watu maarufu, Wakuu wa wilaya ni kundi muhimu kwa vile wao ni Wenyeviti wa kamati wa ulinzi na Usalama katika wilaya zao.
” Watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio vya utalii huzingatia ukalimu na usalama wao na Wakuu wa wilaya ndio wasimamizi wakuu wa Usalama wa watalii pamoja na Mali zao” Alisema. ” Tulianzakuwarumia Waandishi wa Habari, wakafuata wasanii na leo tumekuja na Wakuu wa wilaya lengo letu ni kuona jamii inapata mwamko wa kutembelea vivutio vya wenyewe” alisisitiza.
Amesema Wakuu wa wilaya hao ni viongozi wanaowahakikishia usalama watalii na ndio kwenye jukumu la kuhakikisha kila mtalii anayekuja nchini kutembelea vivutio vya Utalii analala salama na anaamka salama.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo kwa Wakuu wa wilaya, Mhe.Kanyasu amesema ameamua kuanza na Wakuu wa wilaya hao ni wawakilishi wa Wakuu wa Wilaya wenzao kwa vile vivutio vya Utalii vilivyopo nchini vipo katika maeneo hao kazi hivyo lazima watambue fursa zinazopatikana katika vivutio hivyo Aidha, Amesema kwa vile wao ni viongozi ni watu muhimu katika kutumia ushawishi walio hao kwa wananchi wanaowangoza katika kutembelea vivutio vya Utalii.
Kwa upande wake, Damiani Salu ambayeni Mkuu wa Hifadhi hiyo amesema ujio wa Wakuu wa Wilaya hao utasaidia kuchagiza Utalii wa ndani kwa vile wao ni viongozi wanaowangoza watu hivyo watatumia ushawishi wao katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutembelea Hifadhi nchini.
Pia, Mkuu wa Hifadhi hiyo amewaeleza Wakuu wa wilaya hiyo kuwa Hifadhi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuongeza Wanyamapori mbalimbali wakiwemo simba wa kutoka familia tano.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia makundi mbalimbali yenye ushawishi katika jamii katika kuhamasisha Utalii wa ndani ambao umekuwa haufanyi vizuri.
Wakuu wa wilaya waliotembelea Hifadhi hiyo ni Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Mhe. Asiya Abdallah, Mkuu wa wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda, Mkuu wa wilaya ya Momba, Jumaa Irando pamoja na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva.
Wengine ni Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, Mkuu wa wilaya ya Kongwa, Deogratias Ndejembi, Mkuu wa wilaya ya Musoma, Vicent Naano pamoja na Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga.
Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato ni miongoni mwa Hifadhi mpya iliyozinduliwa mapema mwaka huu na Rais John Pombe Magufuli.