Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Wananchi wa Mkuranga wameishukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA chini ya serikali ya Awamu ya Tano kwa kupeleka mradi wa maji katika mji wao unaotarajiwa kumalizika Aprili 2020.

Mradi huo unatarajia unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la Lita 1.5 na utahudumia  Mji wa Mkuranga hadi Vikindu ukiwa ni mrefu wa Km 65 na wananchi zaidi ya 35,000 watanufaika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo amewataka wananchi wa Mkuranga kulinda miundo mbinu na vyanzo vya maji ili waendelee kupata huduma ya maji safi.

Ameyasema hayo leo baada ya kutembelea na kujionea Ujenzi wa tenki la Mkuranga akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo hilo Abdalla Ulega na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zainab Vullu..

Jaffo amesema, wananchi watakapolinda miundo mbinu ya maji na kutoifanyia uharibifu watanufaika na miradi ya maji inayoletwa na Dawasa katika Mji wao.

"Mimi nasema ukweli, tusitake kuwapoteza Dawasa kwa mradi huu waliouleta una thamani kubwa sana utakaoondoa kero ya maji katika mji wetu wa Kisarawe, wananchi hatuna budi kuilinda miundo mbinu ya maji na vyanzi vyake," amesema

Jaffo, "tuwe walinzi wa miradi yetu wenyewe na mimi naipongeza sana Dawasa kwa kutambua kero kubwa ya wananchi ni kupata maji safi kwani jana tulikuwa Jimboni kwangu Kisarawe wamefanya kazi kubwa sana sasa hivi Kisarawe wanafungua maji safi,"

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo hilo, Ulega amesema wamekaa kwa kipindi kirefu wakiwa na changamoto ya maji safi ila kufikia April 2020, wananchi wa Mkuranga na maeneo yake wataanza kupata maji ya uhakika.

"Niwashukuru sana Dawasa wamefanya kazi kubwa sana ya kutuletea huduma ya maji ndani ya Wilaya ya Yetu ya Mkuranga, wananchi wameteseka sana ila kuja kwa mradi huu kutatatua changamoto ya muda mrefu," amesema Ulega.

Amesema, mradi huu ni kwa fedha za ndani ya Dawasa hana budi kuwaasa wananchi wa Mkuranga kulinda vyanzo vya maji na miundo mbinu ya maji katika kipindi chote.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huu una thamani ya Bilion 5.6 zikisa ni mapato ya ndani ya Mamlaka na wametekeleza mradi huu utakaomalizika Aprili mwakani.

Amesema kwa sasa wanaanza kuwasajili wananchj wote wanaotaka huduma ya maji ndani ya Mkoa wa Kihuduma Mkuranga na tayari wameshafungua ofisi na Meneja yupo kazini kila siku.

Mradi wa Mkuranga umekuwa moja ya miradi ya Dawasa iliyosainiwa kwa ajili ya kuondoa changamoto za maji kwenye Maeneo tofauti ya Mikoa ya Kihuduma ya Dawasa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja akielelezea ujenzi wa mradi wa maji wa Mkuranga kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo ( kushoto) , Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdalla Ulega na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zainab Vullu..
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja akielelezea ujenzi wa mradi wa maji wa Mkuranga kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo ( wa pili kulia) , Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdalla Ulega (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zainab Vulla.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo akitoa pongezi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam  DAWASA baada ya kufanikisha mradi wa Mkuranga utakaokamilika Aprili 2020.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Abdalla Ulega akiwapongeza Dawasa kwa kuwezesha Jimbo la Mkuranga kupata mradi wa maji wenye thamani ya Bilion 5.6 Kushoto  ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jaffo na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zainab Vulla, 
Ujenzi wa Tenki la maji ukiendelea.