Mama Mzazi wa mtoto aliyekutwa mtupu, huku Baba yake akiwa ameshikilia Panga na msumeno katika maporomoko ya maji mkoani Morogoro, Marry Shao, amesema kuwa mumewe huyo alianza kubadilika siku za hivi karibuni na kuanza kuongea maneno ya ajabu hadi siku ya juzi alipokamatwa.


Mke wa mwanaume aliyekutwa akiwa mtupu yeye na mwanae katika maporomoko ya maji mkoani Morogoro, Marry Shao

Akizungumza leo Disemba 21, 2019 mkoani Morogoro, Marry amesema kuwa yeye na mumewe wana watoto wawili na tayari ameshakabidhiwa mwanaye.

"Mume wangu alianza kubadilika Novemba 29, 2019 siku ijumaa, kwakweli alianza kuongea mambo ambayo mimi siyaelewi, alikuwa anaongea mambo ya ufalme wa mbinguni, na siku ya tukio alikuwa yuko tu vizuri hadi anaondoka na mtoto alikuwa sawa" amesema Marry.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kumshikilia mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Benson Sadala na kwamba wanaendelea kumfanyia uchunguzi ikiwemo kumpima ili kujua afya yake ya akili.

Tukio hilo lilitokea siku ya Disemba 19 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni na ilidhaniwa kuwa mwanaume huyo alitaka kumfanyia tukio la kihalifu mwanaye mwenye umri wa miaka 7, ambapo alikutwa katikati ya maji yaendayo kasi na alikutwa tayari ameshafanya uharibifu katika vyanzo vya maji kwa kukata mabomba.