Dar es Salaam. Mmiliki wa Kampuni ya Clouds Media ya Tanzania, Joseph Kusaga ameeleza sababu ya nyimbo za msanii nchini humo Diamond kutopigwa wala kuchezwa katika kituo cha redio Clouds na Clouds Tv licha ya kuelekeza wafanyakazi wa vituo hivyo kuzicheza.

Kusaga ameyasema hayo jana Jumatano Desemba 11, 2019  katika mahojiano kwenye kipindi cha Bartender ambapo kati ya maswali aliyoulizwa ni pamoja na kwa nini kituo hicho hakipigi nyimbo za Diamond.

Kusaga amesema chanzo cha nyimbo za Diamond kutopigwa kilikuwa siku moja walipoanza kucheza nyimbo za Mbosso msanii kutoka lebo ya Wasafi.

“Tulipiga ngoma ya Mbosso siku moja, tukaulizwa kwa nini hatujapiga kwa miaka mitano nyimbo za Diamond na kutakiwa kuandika barua ya kujieleza.

“Mimi Kusaga niandike barua kwa nini sijapiga nyimbo zako, kwani napata hasara gani kama ni biashara zangu zinaendelea tu si umetaka nifunguke,” Kusaga alimuuliza mtangazaji huku wakicheka.

Pia, kuhusu sakata hilo alitaka waulizwe uongozi wa wasafi akiwemo meneja wa Diamond, Tale na Salama ambao hata hivyo amesema hana tatizo nao kwani ametoka nao mbali na anaheshimu maamuzi yao.

Mwananchi