Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amezitaka jamii zinazoendekeza mila na desturi, zinazochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi, zikiwemo Vigodoro na Chagulaga kujitafakari.

Waziri Mhagama ameyabainisha hayo leo Desemba 1, 2019, Jijini Mwanza, alipozungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, ambapo amewaomba wadau mbalimbali kuangalia namna ya kuzibadilisha mila hizo ili kuweza kusaidia juhudi za Serikali, katika mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi na Virusi vyenyewe.

"Yako makabila yana Mila za chagulaga, Nyumba Ntobo, kutakasa wajane, kusafisha ghala pamoja na vigodoro ninyi muendelee kujitafakari, hizi mila zote hazituokoi, hazitupelekei kupambana na mambukizi mapya, bali zinatusababisha kuongeza maambukizi mapya na kupelekea  juhudi za Serikali kuendelea kupata changamoto", amesema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi hapa nchini (TACAIDS), Dkt Leonard Maboko, amesema kuwa hadi kufikia leo asubuhi katika viwanja vya Rock City, jumla ya asilimia 6.3 ya waliopimwa Ukimwi, waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, wanawake wakiwa 133 na wanaume 9 kati ya watu 2,265, waliojitokeza kuanzia Novemba 25