MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya K-Finance, Judith Minzi ametaja sababu za biashara nyingi zinazoanzishwa nchini zimeshindwa kuendelea kuwa ni pamoja na kutokujua namna ya kutafuta masoko, kunakili biashara ambayo anafanya mtu bila kujua wazo lake namna lilivyoanzishwa.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania(BOT) kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Sekta ya Fedha(FSDT) kufanya utafiti kujua sababu ya biashara nyingi hasa zinazoanzishwa na wanawake zinashindwa kufikisha miaka mitatu.
Ashatu alitoa maagizo hayo katika mdahalo wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuhusu sekta ya fedha, akiwataka watafute sababu zinazosababisha asilimia 51 ya biashara zinazoanzishwa na wanawake nchini hufa kabla ya kufikisha miaka mitatu.
Akizungumza katika maonesho ya Biashara ya Wanawake yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Judith alisema elimu ya biashara kwa wafanyabiashara wengi ni tatizo hivyo kushindwa kujiendesha.
Alisema changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa wafanyakazi wanaomsaidia mfanyabiashara kuuza bidhaa hiyo kama wanaijua na wanajua maono ya mwanzilishi.
“Ni muhimu kwa wafanyabiashara kutafuta elimu ya biashara kupitia njia mbalimbali ikiwamo mafunzo yanayotolewa na taasisi nyingi hapa nchini,” alisema Judith.
Aliishauri serikali kuanzisha somo la ujasiriamali kwa shule za msingi ili kuwajengea uwezo wanafunzi waweze kukua wakijua namna ya kufanyabiashara.
“Tuendelee kushawishi wanafunzi wapende kusoma somo la hesabu kwani linasaidia katika uanzishaji na usimamizi wa biashara,” alisema Judith.
Alisema kwa kuliona hilo taasisi ya K-Finance imeandaa mafunzo kwa wajasiriamali yatakayofanyika Januari 18, 2020 pale Hekima Garden, Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa kufundisha jinsi ya kutumia vipaji vyako kufikia uhuru wa kiuchumi.
Judith alisema katika uchunguzi walioufanya wamebaini kuwa watu wengi wanaoanzisha biashara wanashindwa kufikia malengo kutokana na kutokuwa na elimu hiyo.
Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwapa uelewa wa biashara wanazofanya na watakazoanzisha ili kuziwezesha kuwa imara na kudumu kwa muda mrefu.“Tutawakutanisha wafanyabiashara waliofanikiwa na ambao ndio wanaanza ili kubadilishana uzoefu na changamoto zinazopatikana katika ufanyaji biashara,” alisema Judith.
Alisema wafanyabiashara wengi waliofanikiwa wamepitia changamoto mbalimbali ambazo wakibadilishana na wanaoanzisha biashara zitawasaidia kujua namna ya kuzitatua watakapokumbana nazo.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yaitwayo ‘Ignite Business Clinic’ yataongozwa na Mchumi Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania(BOT) kwa Zaidi ya miaka 20, na ndiye Mkurugenzi Mwanzilishi wa K-Finance, Bi. Devotha Minzi pamoja na uwepo wa mgeni rasmi aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo na sasa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb)
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya K-FINANCE inayotoa Mikopo na Ushauri wa Kibiashara kwa wafanyabiashara na watu binafsi Judith Minzi (aliyesimama), akipewa maelezo na moja ya washiriki wa maonyesho ya wanawake wajasiriamali maarufu kama Women in Business Balance ambayo yalifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni. K-Finance ilidhamini maonyesho hayo kuongea na washiriki juu ya uhuru wa kiuchumi na vile vile kuhamasisha semina maarufu kama Ignite Business Clinic (IBC) Msimu wa pili ambao utafanyika Januari 18 2020 kwenye ukumbi wa Hekima jijini Dar es Salaam. (Picha na mpigapicha wetu).