Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Adili Elinipenda akionyesha baadhi ya vidhibiti wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu kumkamata Hakimu anayetuhumiwa kwa rushwa ya shilingi 250,000/=.
Na Jumbe Ismailly, SINGIDA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida inamshikilia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mtinko, katika Halmashauri ya wilaya ya Singida kwa tuhuma za kupokea rushwa ya shilingi 250,000/= kutoka kwa mtoa taarifa ili aweze kutoa upendeleo kwenye kesi ya madai inayomkabili katika Mahakama hiyo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda alimtaja Hakimu huyo wa Mahakama ya mwanzo kuwa ni Benard Modest Kasanda na kwamba alitenda kosa hilo Desemba 16, mwaka huu kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

“Mtuhumiwa Hakimu Kasanda alikamatwa na TAKUKURU Mkoa wa Singida baada ya kupokea kiasi cha shilingi 250,000/= kutoka kwa mtoa taarifa ili aweze kutoa upendeleo kwenye kesi ya madai namba 137/2019” alisisitiza mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Singida.

Aidha Elinipenda alifafanua kwamba mtuhumiwa huyo baada kupokea fedha hizo ndipo alizificha kwenye kasha la dawa ya meno aina ya Whitedent.

Mkuu huyo wa TAKUKURU hata hivyo aliweka bayana kwamba baada ya kumpekua zaidi mtuhumiwa walifanikiwa kumkuta na kiasi kingine cha fedha cha shilingi 489,100/= pamoja na visu vitano, huku kimoja kikiwa kwenye soksi,vingine vikiwa kwenye droo ya meza yake na kwenye mkoba wake.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa taasisi baada ya tukio hilo, vile vile wananchi wengine wawili waliodai wana mashauri yao mbele ya mtuhumiwa Hakimu Kasanda walijitokeza kwa Takukuru na kusema nao pia walimpatia mtuhumiwa fedha, huku mmoja akidai kutoa shilingi 50,000/= na mwingine shilingi 200,000/=

Hata hivyo Elinipenda alibainisha kuwa Takukuru inaendelea kuchunguza mashauri haya yote na umma utajulishwa baada ya kukamilika,hivyo basi taasisi hiyo inaendelea kuwakumbusha wananchi wote wa Mkoa wa Singida kutoa taarifa za vitendo vya rushwa mara moja ili hatua za kisheria ziweze kuchukulia kwa wakati.