Mkubwa Fella ambaye ni mmoja wa mameneja wa msanii wa Bongofleva nchini Tanzania, Diamond Platnumz, ameeleza sababu ya kuwataka Clouds Media kutoa maelezo kwa nini walifunga na baadaye kufungulia kupiga nyimbo za wasanii wa lebo ya WCB.

Fella ameyasema hayo ikiwa ni siku chache tangu Mkurugenzi wa kampuni ya Clouds Media, Joseph Kusaga kusema kuwa waliamua kuacha kabisa kupiga nyimbo za wasanii wa lebo hiyo baada ya kutakiwa kuandika barua ya maelezo na viongozi wa lebo hiyo.

Kutokana na hilo Mwananchi ilitaka kujua maoni ya Fella kuhusiana na hilo na kama bado wataendelea kushikilia msimamo wao.

Katika maelezo yake Fella ambaye jina lake halisi ni Said Fella, amesema walifikia hatua hiyo kutokana na kitendo cha kutopigwa kwa nyimbo za Diamond ambako hakukumuathiri Diamond mwenyewe bali na watu walioko nyuma yake.

Akifafanua, Fella amesema iliwauma kuona kama ni Diamond walitaka kumfungia kwa nini wakajumuishwa na wasanii wengine ambao hawakuwa na kosa lolote.

“Msanii kama Lavalava maskini ya Mungu alikuwa na kosa gani la kutochezwa kwa nyimbo zake, yaani kisa tu bosi wake Diamond hamtaki kumpigia nyimbo zake, huyo Mbosso mwenyewe tangu anatoka hawakuwahi kumpigia, ndio maana walipojaribu kucheza wimbo wake tulitaka kujua sababu ya wao kuanza kupiga nyimbo za wasanii wetu.

“Mlitufungia hatukujua sababu hasa ni nini na mkatufungulia bila kujua nini kilichowasukuma, sasa yote haya tuimetaka kujua sababu ili kila mtu ajue kosa lake na hatukua na nia nyingine mbaya,” amesema mkubwa Fella.

Fella amesema wanachoshukuru pamoja na Diamond kubaniwa na baadhi ya redio na TV kutochezwa kwa nyimbo zake, ndio kwanza anazidi kung’aa na kuvitaka vyombo hivyo kujitafakari mara mbili huenda vyenyewe ndio havina umaarufu.

Pia amesema anashukuru kwa ujio wa mitandao ya kijamii kwani imewasaidia kuacha tabia za kunyenyekea watu kucheza nyimbo za wasanii wao na kuhoji nani leo angejua kwamba Diamond anafahamika vilivyo nchi za Magharibi ambapo alikuwa huko kwa ziara ya kimuziki.