Mwanaume mmoja amevamia benki ya Academy iliyoko Colorado nchini Marekani na kuiba fedha, kisha akazirusha zote kwa wapita njia akipaza sauti kuwatakia heri ya Sikukuu ya Krismas.
BBC imeripoti kuwa polisi walimtaja mtuhumiwa huyo kwa jina la David Wayne Oliver mwenye umri wa miaka 65, aliyekuwa na ndevu ndefu nyeupe. Imeelezwa kuwa alifanya tukio hilo Jumatatu, Desemba 23, 2019.
“Alivamia Benki ya Academy na kuiba fedha, akatoka nje na kuzirusha zote kwa wapita njia zikasambaa,” shuhuda mmoja amekaririwa na chombo cha habari cha Colorado cha 11 News.
“Alianza kuzirusha pesa zote hewani akizitoa kwenye begi, na alipiga kelele, ‘Merry Christmas!’,” aliongeza shuhuda huyo.
Hata hivyo, Polisi wameeleza kuwa wapita njia walifanya jambo jema, wakaziokota fedha hizo na kuzirejesha tena ndani ya benki
Shuhuda ameeleza kuwa Oliver alikimbia hadi mbele ya duka la kahawa, akakaa mbele ya duka hilo akisubiri kukamatwa. Polisi walimkuta hapo na kuondoka naye.