WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wasanii nchini humo kufanya juhudi katika kazi zao za sana ili waweze kupata mitaji ya kuwawezesha kuanzisha biashara nyingine.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa, Novemba 15, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la sanaa la Mwalimu Nyerere liliandaliwa na mashirikisho ya wasanii Tanzania.

Waziri Mkuu amesema wasanii wakifanya kazi zao kwa umahiri zitauzika na wataweza kupata fedha za kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi. Akimtolea mfano msanii Shilole amemtaja kama mfano bora kwa wasanii waliojikwamua kiuchumi kwa kuanzisha biashara ya mgahawa wa chakula.

“Nilimuona Shilole kwenye TV (Televisheni) anasema mtaji wake aliopata kuanzisha biashara umetokana na kazi ya sanaa, nampongeza kwa hilo.”

“Niwasihi wasanii hii iwe mfano, fanyeni kazi mpata mitaji muanzishe biashara nyingine nje ya sanaa mtafanya vizuri pia upande huo,” amesema. Majaliwa pia amewataka wasanii kuacha migogoro isiyo na msingi na badala yake wajikite katika kuinuana na kuendelezana.