Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela wakati wa Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni Kanda ya Kusini.
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akitambulishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (katikati) kwa Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRD Dkt. Joseph Witts wakati alipowasili kufungua Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni Kanda ya Kusini lililofanyika Mkoani Mtwara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akihutubia wakati wa Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni Kanda ya Kusini.
David Jere, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi (CRDB) akihutubia wakati wa Kongamano la Uwezeshaji kwa Wakandarasi na Wazabuni Kanda ya Kusini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi kutumia mabenki kuchukua mikopo ili kuwawezesha kukamilisha miradi yao kwa wakati na kuacha kutegemea malipo ya awali ya mradi husika ambazo zimekuwa zikichelewa na kufanya miradi kutokamilika kwa wakati.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika kongamano lililo andaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wakandarasi ,wazabuni na wafanyabishara wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, lilifanyika katika ukumbi wa Benki Kuu, mjini Mtwara. Kongamano hilo lililenga kuwapatia washiriki hao elimu juu ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazozichukua kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, wakandarasi ni sekta muhimu sana katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini hivyo wanapaswa kuboresha utendaji kazi wao kwa kuchukua mikopo toka taasisi za fedha na mabenki. Ameongeza kuwa, changamoto kubwa inayowakabili wakandarasi wengi ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ambapo changamoto hiyo huchangia kutomalizika kwa miradi kwa wakati.

“Benki ya CRDB imewaletea fursa mlangoni, itumieni vilivyo, changamkieni fursa hizo ili muweze kukuza biashara zenu na kupata faida zaidi, kuongeza ajira kwa vijana wetu na hatimaye kulipa kodi stahiki za serikali. Ni matarajio yangu kuwa, baada ya kongamano hili tutaona utofauti mkubwa kutoka kwa wakandarasi na halmashauri, ambao wamekuwa wakipitia changamoto katika kukamilisha miradi yao, kutokana na suala la mapato na ukwasi” alisema Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Majaliwa pia alipongeza benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa miondombinu mbalimbali ambayo itasadia kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alisema “Benki ya CRDB imekuwa ina fadhili miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika jitihda zake za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Tunatambua na kuthamini sana ushikiri wa Benki ya CRDB katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa maji katika bonde la Rufiji (Nyerere Hydro Power Project) na ule wa kusambaza nishati ya umeme vijijini yaani REA.

Kipekee kabisa niwapongeze tena Benki ya CRDB kwa utayari wenu, ambao mmekuwa mkiuonesha katika kuisaidia Serikali, hususan katika utekelezaji wa miradii mikubwa ya kimkakati”. alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema kuwa,kongamano hili ni fursa pekee ya kuwakutanisha wakandarasi, wazabuni na wafanyabisahra ili kuwajengea uwezo na kuwajulisha fursa mbalimbali za kifedha zilizomo ndani ya benki ya CRDB, na namna ya kuzitumia fursa hizo ili kukuza miradi na biashara zao.

“Tuna bidhaa nyingi mahususi kwa ajili ya kundi hili la wateja ikiwamo: Purchase Order Financing, Contract financing, and Invoice Discounting ambazo hazihitaji dhamana yoyote kutoka kwa Mkandarasi au mzabuni pindi anapotaka kukopa. Zaidi ya hilo, Benki pia hutoa mikopo kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi, magari, mashine, Mabasi na huduma nyingine kama vile dhamana ya malipo ya awali (Advance Payment Guarantee), dhamana ya Utekelezaji wa Miradi (Performance Guarantee), Barua za Mikopo (Letters of Credit), Huduma za Bima na pia tunatoa mikopo ya muda mfupi kama mitaji ya kufanyia kazi” alisema.

Naye mmoja wa Wakandarasi Henry Shimo ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Chibeshi constructions Ltd , amesema kuwa, swala zima la uwezeshwaji wa mikopo hiyo litawasaidia kwa kiasi kikubwa sana wakandarasi hao kumaliza miradi yao kwa wakati kwani changamoto kubwa ilikuwa ni mitaji kwa ajili ya kuendeleza miradi yao. Amesema kuwa, kinachotakiwa kikubwa ni uaminifu wa wakandarasi katika kujua fedha wanayopewa inahitaji kufanyiwa kazi na kurudishwa kwa wakati.