Watu sita wameuawa katika kijiji cha Ngongo Wilaya ya Tandahimba mkoani  Mtwara na wengine saba kujeruhiwa katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Jumanne Novemba 12, 2019.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema Watanzania sita walipigwa risasi na watu wanaodhaniwa kutoka nchi jirani ya Msumbiji wakati wakiwa visiwa vya mto Ruvuma wanakofanya shughuli za kilimo.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vitahakikisha wahalifu hao wanapatikana na sheria kali zitachukuliwa juu yao, niwasihi tu wananchi kuepuka kwenda nchi za watu bila kuwa na vibali,” amesema.

Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Leberatus Sabas, amesema kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ndio maana wahalifu wanafanya matukio hayo mipakani.

“Tusikubali hata siku moja wavuke mpaka waje huku ndani tupo bega kwa mbega na wananchi. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo pamoja tutawasaka, tutawatia mbaroni na hatua kali zitachukuliwa.”